Zaidi ya Sh bilioni 52 zimetumika katika ujenzi wa Mahakama za Mwanzo 60 katika mikoa mbalimbali hapa nchini na ifikapo Juni mwaka huu kazi itakuwa imekamilika.
Taarifa hizo zimetolewa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama Tanzania Prof Elisante Ole Gabriel wakati akizungumza na waandishi wa habari jana katika viwanja vya Mahakama Kuu Kanda ya Geita iliyopo Bomani mkoani hapo.
Gabriel alisema katika mkopo wa awamu ya pili kutoka benki ya Dunia ujenzi wa Mahakama za Mwanzo 60 katika mikoa mbali mbali hapa nchini na gharama za ujenzi ni bilioni 52.3 na tunategemea ifikapo Juni mwaka huu kazi itakuwa imekamilika.
Pia Gabriel ameipongeza serikali kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa Mahakama katika mikoa mbalimbali hapa nchini.
Alisema ili kutambua serikali inawekeza ndani ya mahakama bajeti yao ilikuwa ni Sh bilioni 241 na bajeti iliyopitishwa na Bunge ni bilioni 321.
Alisema jengo la Makao Makuu Dodoma ni jengo la kifahali, jengo la historia, jengo la Sita kwa ukubwa Duniani na sasa nchi mbali mbali zinakuja kufanya utalii katika jengo hilo ambalo juu yake kuna uwanja wa kutua Helukoputa.
Alisema zamani majengo ya mahakama yalikuwa yamechoka choka sana lakini sasa hivi majengo yote ya mahakama katika mikoa mbali mbali hapo nchini ni mazuri na yanapendeza na yana huduma za watu wenye ulemavu.
“lengo letu ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa wakati na kwa haraka zaidi, tofauti na hapo zamani na kuepusha gharama kwa wananchi wanaokuja kupata huduma hapa mahakamani”alisema.
Aidha aliwataka wananchi kufurahia huduma ya Tehama lengo ni kuboresha huduma kwa haraka na kufanya wananchi wapate huduma kwa haraka na kurudi majumbani mwao kufanya kazi zao kwa wakati.
Alisema kwa sasa jengo moja linachukua Mahakama ya Mwanzo, Mhakama ya Wilaya, Mahakama ya Hakimu Mkazi, Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa lengo ni kumpunguzia mwananchi usumbufu wa kufata huduma sehemu mbali mbali, lakini kwa sasa huduma zote zinapatikana kwenye jengo moja.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED