Wahitimu wa SUA watakiwa kutumia elimu kuleta mabadiliko

By Christina Haule , Nipashe
Published at 04:32 PM May 22 2025
Wahitimu wa SUA watakiwa kutumia elimu kuleta mabadiliko
Picha: Mpigapicha Wetu
Wahitimu wa SUA watakiwa kutumia elimu kuleta mabadiliko

Wahitimu 794 wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wametakiwa kutumia elimu waliyoipata kwa kuweka alama ya mabadiliko chanya katika jamii, kwa kutazama maisha kwa mitazamo ya kitaaluma katika dunia inayobadilika kutokana na mazingira.

Wito huo umetolewa leo na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha SUA, Andrew Massawe, wakati wa mahafali ya 45 ya chuo hicho, yanayoongozwa na Mkuu wa Chuo, Profesa na Jaji Mstaafu Joseph Sinde Warioba.

Massawe amesema kuwa mabadiliko ya maisha yaliyopo yakitumiwa kwa namna sahihi, huweza kuwa chanzo cha fursa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kujiajiri na kuwaajiri wengine.

“Mitazamo ya kitaaluma ni msingi muhimu kwa maisha ya sasa. Mabadiliko hayakwepeki, lakini yakitumika kwa hekima, huibua fursa mpya za maendeleo,” amesema Massawe.

Aidha, alibainisha kuwa katika mahafali ya 44 yaliyopita, Baraza la Chuo lilipitisha maamuzi kadhaa muhimu, likiwemo lile la kuongeza wigo wa mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi ili kuhakikisha wanakuwa na uwezo wa kukabiliana na mazingira ya kazi wanapohitimu.

Kwa upande wake, Makamu wa Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Raphael Chibunda, amewakumbusha wahitimu hao kuwa kuhitimu kutoka SUA si jambo rahisi, bali ni matokeo ya juhudi, nidhamu na kujituma.

“Kupitia SUA si lelemama. Mmeonyesha juhudi kubwa na dhamira ya kweli. Nawapongeza kwa mafanikio haya makubwa. Vilevile nawapongeza wazazi na walezi kwa mchango wao mkubwa katika safari yenu ya elimu,” amesema Prof. Chibunda.

Katika mahafali hayo, jumla ya wahitimu 794 walitunukiwa shahada na astashahada mbalimbali, wakiwemo wahitimu wa Shahada ya Kwanza, Shahada ya Umahiri na Shahada ya Uzamivu (PhD). Kati yao, wanaume walikuwa 495 na wanawake 299, sawa na asilimia 37.7.


2