Maelfu ya wakulima wilayani Iramba wameanza kunufaika na mbinu bora za kilimo chenye tija kupitia Mradi wa Lishe uitwao NOURISH, unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Norway (Norad) na kutekelezwa na SNV kwa kushirikiana na Farm Africa kupitia mashirika ya Recoda na Miico.
Kupitia mradi huo, umeandaliwa Siku ya Wakulima kwa lengo la kuboresha usalama wa chakula, kusaidia jamii kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na kupunguza tatizo la utapiamlo.
Akizungumza katika kijiji cha Ngalagala, Afisa Mradi, Salome James, amesema kuwa NOURISH umesaidia jamii kukabiliana na changamoto mbalimbali za kilimo ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya tabianchi na miundombinu duni.
“Katika kipindi cha mwaka mmoja tu, zaidi ya bustani 310 za mbogamboga zimeanzishwa, vikundi 59 vya wakulima vimeundwa na mashamba darasa 174 yameanzishwa,” amesema Salome.
Aidha, amesema mbegu bora pamoja na viazi lishe vimesambazwa kwa wakulima, huku wakulima 320 wakifanyiwa upimaji wa afya ya udongo ili kuongeza uzalishaji kwa tija.
Kwa upande wake, Ofisa Tarafa wa Iramba, Charles Makala, amewahimiza wakulima kutumia kikamilifu teknolojia na maarifa waliyopatiwa kupitia mradi huo kwa maendeleo ya jamii zao.
“Maarifa haya yasiishie kwenye mashamba darasa pekee, bali yaendelezwe hadi mashambani kwa wakulima wote kwa manufaa ya familia na taifa,” amesema Makala.
Mradi wa NOURISH unatekelezwa katika mikoa mitano ya Dodoma, Manyara, Rukwa, Singida na Songwe, kwa kipindi cha miaka mitano, ukiwa na lengo la kuimarisha usalama wa chakula na ustahimilivu wa jamii dhidi ya athari za tabianchi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED