Madini ya vito, makaa ya mawe na dhahabu yameelezwa kuwa kichocheo kikuu cha uchumi katika Mkoa wa Ruvuma, huku yakisaidia kuongeza makusanyo ya maduhuli ya serikali hadi kufikia asilimia 98 ya lengo kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Ruvuma, hadi kufikia Mei 19, 2025, mkoa huo ulikuwa umeshakusanya Shilingi bilioni 32.5 kati ya lengo la Shilingi bilioni 33.15, na matarajio ni kuvuka lengo hilo kufikia mwisho wa mwaka wa fedha Juni 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari wa Tume ya Madini, Mhandisi Alphonce Bikulamchi amesema mafanikio hayo yametokana na kushamiri kwa biashara ya makaa ya mawe, ambayo kwa sasa yanauzwa katika nchi mbalimbali zikiwemo Kenya, Uganda, Rwanda, na hata kufika Bara la Asia na Ulaya.
“Ruvuma imebarikiwa kuwa na aina nyingi za madini. Mbali na makaa ya mawe, kuna dhahabu, shaba, chuma, urani, madini ya ujenzi na madini ya vito,” alisema Mhandisi Bikulamchi.
Aidha, ameeleza kuwa serikali kupitia Tume ya Madini imeanzisha masoko mawili ya madini, ikiwemo Soko la Madini Songea na Soko la Madini Tunduru, ambayo yamechangia kuongeza uwazi, ulinzi wa haki za wachimbaji na kukuza mapato ya serikali.
Mhandisi Bikulamchi ametoa wito kwa Watanzania kuchangamkia fursa zinazotokana na sekta ya madini ikiwa ni pamoja na:
“Huu ni wakati muafaka kwa Watanzania kushiriki kikamilifu katika uchumi wa madini kwa kutumia fursa zilizopo Ruvuma,” alisisitiza.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED