Makalla amwombea mbunge asihukumiwe kisa barabara

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 12:19 PM May 22 2025
Erick Shigongo.
Picha:Mpigapicha Wetu
Erick Shigongo.

Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM, CPA Amos Makalla, amewataka wananchi wa Buchosa wasimhukumu mbunge wao, Erick Shigongo, kutokana na kutokamilika kwa barabara ya Sengerema- Buchosa, iliyoko Halmashauri ya Buchosa, wilayani Sengerema, mkoani Mwanza.

Makalla ametaja sababu ya kutokukamilika kwa barabara hiyo yenye urefu wa takribani kilomita 53 inayojengwa kwa kiwango cha lami ni kutokana na kazi ya mkandarasi aliyekabidhiwa awali haikuridhisha ndipo alipoondolewa, lakini taratibu za kumpata mwingine zimekamilika.

Akizungumza Mei 21, 2025,  na wananchi Halmashauri ya Buchosa, wilayani humo, Makalla aliyeko katika ziara ya kikazi ya siku saba, katika mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza Simiyu na Shinyanga anasema anaifahamu barabara hiyo tangu akiwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.

“Barabara Sengerema-Buchosa naomba Erick asihukumiwe nayo ninaijua vizuri, nilikuwa Mkuu wa Mkoa huu nimeshiriki baada ya mkandarasi kuzingua nilisema mkandarasi afutwe kazi ili wizara tupate mwingine. 

“Ninajua ni mambo ya kisheria hatimaye ameondoka ninajua Waziri Mkuu alikuwa hapa na Waziri baada ya kupatikana mkandarasi barabara itamalizika,” amesema.

Makalla amesema ameamua kulisema hilo ili isiwe fimbo kwa wanasiasa wengine.

“Tulifanya uamuzi mgumu kwa maslahi ya wananchi wa Buchosa ili barabara isilipuliwe,” amesema.