PDPC yaja na mpango kukabiliana na udukuzi

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 03:16 PM May 22 2025
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume hiyo, Mhandisi Stephen Wangwe .
Picha: Mpigapicha Wetu
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume hiyo, Mhandisi Stephen Wangwe .

Siku chache baada ya baadhi ya akaunti za mitandao ya kijamii kudukuliwa, Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), imetangaza kuanza kwa mpango wa mafunzo maalum kwa Maofisa ulinzi wa taarifa binafsi kutoka taasisi zote za umma na binafsi mwezi ujao yatakayosaidia kukabiliana na tatizo hilo.

Akizungumza leo na waandishi wa habari jijini Dodoma, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume hiyo, Mhandisi Stephen Wangwe amesema mafunzo hayo yatawapa mbinu za kusimamia ulinzi wa taarifa kwenye maeneo yao kwa kuwaeleza Maofisa hao na wanaosimamia mitandao namna ya kuepukana na kuingiliwa kwenye akaunti.

Mkurugenzi huyo amesema mafunzo hayo yatasaidia kuongeza ustawi wa haki ya faragha na usalama wa taarifa binafsi za watu na kuwezesha Tanzania kuingia rasmi kwenye ulimwengu wa kistaraabu.

“Tutaingia kwenye ulimwengu wa kuhakikisha faragha za watu na usalama wa taarifa za kila mtu zinalindwa, kwasababu heshima zetu zipo kwenye namna ambayo taarifa zetu zimehifadhiwa.”


 “Kutokana na hivi karibuni baadhi ya akaunti za taasisi kudukuliwa hili nalo linagusa upande wa ulinzi wa taarifa binafsi lakini ukiliangalia hasa ni kosa la kimtandao wamechukua utambulisho ambao si wa kwao,”amesema.