Katika kuadhimisha Wiki ya Jumuiya ya Wazazi, Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Bagamoyo imefanya ziara ya maendeleo kwa kutoa msaada wa matofali 1,000 na mifuko ya saruji kusaidia ujenzi wa Zahanati ya Kondo, iliyopo Kata ya Zinga, ikiwa ni juhudi za kuwasogezea huduma za afya wananchi na kuondoa kero ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma hizo.
Aidha, Jumuiya hiyo imezindua mradi wa duka la jumla na rejareja litakalouza bidhaa mbalimbali zikiwemo nguo za chama, vifaa vya matumizi ya ndani pamoja na kufungua shina la wakereketwa la Kibulu la wafugaji, ikiwa ni mikakati ya kuinua uchumi wa jumuiya.
Akihutubia katika maadhimisho hayo yaliyofanyika katika viwanja vya Mnada wa Mbuzi na Ng’ombe kata ya Zinga, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bagamoyo, Abubakari Mlawa, ambaye alikuwa mgeni rasmi, aliipongeza jumuiya hiyo kwa kutekeleza Ilani ya CCM kwa vitendo kupitia miradi ya vitega uchumi.
“Nimefurahishwa sana na ubunifu wa Jumuiya ya Wazazi Zinga. Kufungua duka kubwa la nguo na vifaa ni hatua kubwa ya kujitegemea. Kata nyingine zifuate mfano huu,” alisema Mlawa.
Katika kuunga mkono juhudi hizo, Mlawa alichangia mabati 72 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya Katibu wa Jumuiya ya Wazazi pamoja na kuahidi kuongeza mtaji wa bidhaa katika duka la jumuiya.
Kwa upande wake, Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Bagamoyo, Halima Dosa, alisema lengo kuu ni kuhakikisha kila kata inakuwa na miradi ya kiuchumi itakayowawezesha kujitegemea.
“Tunajivunia hatua ya Kata ya Zinga kwa kusaidia jamii yao – wameanza vyema na tumejipanga kueneza mafanikio haya kata nyingine,” alisema Dosa.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Kata ya Zinga, Hassan Kashingo, alieleza kuwa wameweka mikakati ya kuanzisha miradi mingi ya maendeleo itakayochochea uchumi wa wanajumuiya na kata kwa ujumla.
Katika kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025, Jumuiya hiyo imeapa kushiriki kikamilifu katika kuhamasisha wananchi kujitokeza kujiandikisha na kupiga kura kwa wingi, kwa lengo la kuhakikisha ushindi mkubwa kwa Rais wa Awamu ya Sita, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na CCM kwa ujumla.
Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama, jumuiya zake, serikali na wananchi kutoka kata zote 11 za Wilaya ya Bagamoyo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED