Malima: Wananchi jiandaeni kushiriki uchaguzi

By Christina Haule , Nipashe
Published at 02:00 PM Apr 19 2025
Washiriki mkesha wa Mwenge uliofanyika katika wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro
PICHA: MTANDAO
Washiriki mkesha wa Mwenge uliofanyika katika wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro

MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima amehimiza watanzania kujiandaa na kushiriki uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 bila kuwa na wasiwasi unaoletwa na wachache kuwa uchaguzi huo haupo.

Malima amesema hayo kwenye mkesha wa Mwenge wa uhuru 2025 unaofanyika Wilayani Kilosa mkoani hapa na kwamba uchaguzi ni haki ya kila mmoja kwa mujibu wa katiba hivyo jamii haina budi kujiandaa.

Anasema  ni vema kila mtu kujitokeza kupiga kura huku akiwa tayari amehakiki kitambulisho chake cha kupiga kura na kuwa na umri wa miaka kuanzia 18 ili kumchagua Rais, Mbunge na Diwani wa kumuagiza kuleta maendeleo kwenye eneo lake..

" Uchaguzi upo kama kawaida na wanaosema uchaguzi haupo sisi hiyo hatujui, tuendelee kujiandaa kushiriki uchaguzi mkuu tarehe itakapotangazwa" anasema.

Akizungumza katika sherehe hizo mkimbiza mwenge wa uhuru kitaifa 2025 Ismail Ali Ussi amesisitiza wananchi kudumisha amani na upendo ambao huondoa chuki hasa katika kipindi cha uchaguzi.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka amesema Mwenge wa Uhuru umekimbizwa wilayani humo kwa umbali wa Kilometa 290 sambamba na kukagua na kuweka mawe ya msingi, kuzinduliwa na kuona miradi mbalimbali ya maendeleo.

Shaka amesema Mwenge wa Uhuru utapita katika miradi saba yenye jumla ya  thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 1.82 ambapo miradi iliyopitiwa ni pamoja na mradi wa Barabara, Maji, Afya, Elimu, Mazingira, Kilimo na Maendeleo ya jamii