Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye pia ni Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) na Mbunge wa Mbeya Mjini, Dk. Tulia Ackson, leo Aprili 18, 2025, ameongoza hafla ya uzinduzi wa awamu ya kwanza ya ujio wa mabomba ya maji yatakayotumika katika mradi mkubwa wa usambazaji maji wa Mto Kiwira.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Dk. Tulia amesema mradi huo ni sehemu ya mafanikio makubwa yanayoendelea kuletwa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, katika kuboresha huduma za kijamii kwa wananchi.
“Leo ni siku ya furaha kubwa kwa wananchi wa Mbeya. Huu ni mwanzo wa mwisho wa kero ya muda mrefu ya maji. Tunamshukuru sana Mhe. Rais Samia kwa kusikia kilio chetu na kulifanyia kazi,” amesema Dk. Tulia.
Mradi huo wa maji wa Mto Kiwira unatarajiwa kuwa mkombozi wa mamia ya wakazi wa Jiji la Mbeya na maeneo jirani, ambao wamekuwa wakikumbwa na changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa matumizi ya kila siku.
Awamu hii ya kwanza imehusisha ujio wa mabomba maalum yatakayosambaza maji kwa umbali mrefu, hatua inayofuata ni uunganishaji na usambazaji wa huduma katika maeneo husika.
Mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa dira ya maendeleo ya Taifa inayolenga kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora za msingi ikiwemo maji, afya na elimu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED