Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), limetaka uchunguzi wa haraka na taarifa za wazi zisizo na upotoshaji kwa tukio la kushambuliwa na kuumizwa kwa Katibu wake,Padri Dk.Charles Kitima,ili kurudisha imani na matumaini kwa watu.
Aidha,TEC imesema inashukuru ushirikiano wanaoupata serikalini na vyombo vya usalama.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotoleo leo Mei 1,2025, na Makamu Rais TEC, Askofu Eusebius Nzigilwa kuwa wanalaani tukio baya la uovu la kuvamiwa,na kujeruhiwa kwa Pardi Kitima na kwamba alipata majeraha makubwa na ameleza Hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam.
"Tunawashukuru wote waliosaidia na kumfikisha Padri Kitima hospitalini mapema na kwa madaktari na wauguzi wanaomhudumia mapaka sasa,"amesema.
"Tunatoa wito kwa Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama kuchukua hatua za haraka za kuwabaini na kuwakamata wale wote waliohusika katika kupanga na kutekeleza uhalifu huu wa kinyama na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria,"amesema.
Askofu Nzigilwa amewashukuru watu binafsi, taasisi za ndani na za kimataifa zinazoendelea kulaani na kutupa pole kwa tukio hili baya na la aibu kwa Taifa letu.
"Tunaomba Waamini na watu wenye mapenzi mema muendelee kumuombea neema ya uponyaji Padre Kitima, na pia kuliombea Taifa letu amani na umoja,"amesema.
Aidha, amewaomba wawe na subira na uvumilivu wakati tukisubiri matokeo ya uchunguzi wa vyombo vinavyohusika.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED