Bashe atoa maagio kwa Bodi ya Leseni za Ghala

By Renatha Msungu , Nipashe
Published at 06:15 PM May 01 2025
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe akizungunza na wadau wa zao la korosho k
Picha: Renatha Msungu
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe akizungunza na wadau wa zao la korosho k

SERIKALI imeiagiza Bodi ya Usimamizi wa Leseni za Ghala nchini, kutowapa leseni watunza ghala wanaotoza tozo ya upungufu wa uzito wa korosho ghafi, zilizohifadhiwa ghalani, ili wakulima na wanunuzi wapate haki zao.

Aidha, Waziri wa Kilimo, Bashe amewataka waendesha maghala hao, kuacha tabia hiyo mara moja na endapo watabainika hatua kali za kisheria zitachikuliwa dhidi yao, huku akisisitiza wale waliobainika na makosa hayo wachukuliwe hatua.

Bashe ametoa agizo hilo, jijini Dodoma katika mkutano na wadau wa zao la korosho wakati wakijadili mikakati ya kuikuza sekta hiyo, ikiwamo kufanya tathmini ya zao la korosho katika msimu wa 2024/2025.

Amesema, serikali haitawafumbia macho wasimamizi wa leseni za maghala wasiokidhi vigezo, huku serikali ikiweka bayana mikakati ya kuimarisha zao la korosho, ili kuzidi kuwainua wakulima wa zao hilo kiuchumi na taifa kwa ujumla

"Bodi msiwapatie leseni watunza ghala wa zao la korosho wasiowaaminifu, kwani wanarudisha nyuma wakulima na wanunuzi wa zao hilo hapa nchini," amesema Bashe.

Amesema serikali haitatoa leseni kwa waendesha maghala wanafanya vitendo hivyo, si sahihi na sio vya kiungwana kwa wakulima wanaolima zao hilo kwa sababu watu hao wanalengo la kuwarudisha nyuma.

Bashe amesema mapinduzi yaliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan katika sekta ya kilimo hususani kwenye mazao ya biashara na chakula, yameongeza uzalishaji wa korosho hadi kufikia zaidi ya tani laki tano, tofauti na ilivyokuwa awali.