Wakandarasi wasio na uwezo waivuruga Hai

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 01:16 PM May 01 2025
Kamanda wa TAKUKURU, Wilayani humo, Josiah Gunda.

Wakandarasi ni tatizo Hai. Ndivyo inavyoweza kuelezwa, baada ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, kubaini wakandarasi wasio na uwezo na ambao hawafahamiki, wala kuwa na rekodi ya kazi hiyo, wanapata kazi ya kutekeleza miradi ya ujenzi katika shule za sekondari.

Miradi inayotajwa kuwa na changamoto katika Wilaya hiyo, ni ile ya Shule ya Sekondari Saashisha (milioni 479), Mbatakero (milioni 584), Mkalama (milioni 584) na Mkombozi (milioni 584), ikidaiwa kutekelezwa na wakandarasi wasio na uwezo. 

Akizungumza jana (Aprili 30, 2025) katika kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani la Wilaya hiyo, Kamanda wa TAKUKURU, Wilayani humo, Josiah Gunda alisema: “Fedha hizi zikitumika vibaya itakuwa ni doa kubwa kwenu, sio tu doa, wananchi watapata shida kweli, kwa sababu fedha hizi ni nyingi, ni huruma ya mama Samia, tumeletewa na Mheshimiwa Rais, sasa ziwasaidie wananchi. Wananchi wanahitaji kuona huduma bora kwa wakati lakini sio mabishano yetu na mkandarasi, hayatufai.” 

Akifunga kikao hicho, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Edmund Rutaraka, alisema miradi ambayo imetajwa na Kamanda wa TAKUKURU, ni kweli kuna tatizo, ambako wakandarasi wamepewa kazi hiyo. 

“Jambo jingine ambalo ningependa kuzungumzia ni miradi ya maendeleo, ambayo imeendelea kuonekana kuna sehemu inasuasua, na sio kaliba ya Halmashauri yetu. Sisi Halmashauri yetu miaka yote miradi ikija inafanywa, value for money (thamani ya fedha) inaonekana.


Kwa hiyo miradi hii ambayo imetajwa na Kamanda wa TAKUKURU, kweli kuna tatizo, ambako wakandarasi wamepewa kazi hiyo. Kila siku nazungumza kwenye vikao vyetu nikiwaambia watu wa PMU, User Department na Engineer, wasipofanya kazi kwa pamoja, kwa karibu kuna sehemu wanaweza kuteleza.

 Kwa sababu miradi hii mwanzoni ilivyokuja kwamba kuna fedha ikishazidi fedha fulani hivi hawawezi kufanya force account lakini sasa hivi kuna waraka umekuja, ambao unaelekeza hata milioni 500 wanaweza kufanya force account. 

Na sisi force account tumeona walivyofanya vizuri. Kwa hiyo mkanganyiko wa kubadilisha umekuja kutuletea shida, kwamba tumeenda kwa wakandarasi lakini hawajafanya vizuri kama ilivyotarajia. Sisi tuliamini tukiwapa kazi wakandarasi ilikuwa rahisi kuwa manage na kuwa monitor lakini wakandarasi wengi waliopewa kazi kwenye miradi hii inaonekana uwezo wao ni mdogo. 

Kwa hiyo Mkurugenzi na timu yako, nendeni na timu yako inayohusika, PMU, User Department na Engineer. Mkiwa mnatangaza kazi hizi twende tujiridhishe, tufanye ‘due deligency’ ya wakandarasi hawa tunaowapa kazi, mafundi tunaowapa kazi je wana historia ya kufanya kazi hizi, je wana uwezo wa kufanya kazi hizi, je wana uwezo in terms ya human resources au financial muscles kama anaweza kufanya kazi hizi.