Muuguzi wa Zahanati ya Kijiji cha Malembeka kilichopo wilayani Bunda, Mkoa wa Mara, Zawadi Kazi, amefariki dunia baada ya kujeruhiwa vibaya kwa kuchomwa visu sehemu mbalimbali za mwili wake na mtu anayedaiwa kuwa ni mpenzi wake, Ndege Makebe, kufuatia ugomvi wa kimapenzi.
Baada ya kutekeleza tukio hilo, mtuhumiwa huyo alikimbia na baadaye mwili wake ulikutwa ukining’inia kwenye mti akiwa amejinyonga kwa kutumia shuka la Kimasai.
Akizungumza kwa njia ya simu, Mwenyekiti wa Kijiji cha Malembeka, Ramadhani Sarima, alisema tukio hilo la kikatili lilitokea Mei 1, 2025 majira ya saa 4 usiku. Alisema marehemu alichomwa visu zaidi ya mara kumi katika maeneo mbalimbali ya mwili wake, ikiwemo shingoni, tumboni, ubavuni (upande wa kulia na kushoto), na kwenye matiti yote mawili, hali iliyosababisha apoteze damu nyingi na hatimaye kufariki dunia.
Sarima alieleza kuwa baada ya kufanya mauaji hayo, mtuhumiwa alitoroka kutoka eneo la tukio, lakini baadaye alikutwa amejinyonga kwenye mti kwa kutumia shuka la Kimasai.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Pius Lutumo, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa jeshi la polisi lilikuwa njiani kuelekea eneo la tukio kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED