Vivuko vitano kuanza kazi hivi karibu Ziwa Victoria

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 03:40 PM May 02 2025
Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msingwa (katikati)akiwa ziara mkoani Mwanza kukagua ujenzi wa Vivuko Vitano ambavyo vinajengwa na Kampuni ya Songoro Marine Transport
Picha:Marco Maduhu
Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msingwa (katikati)akiwa ziara mkoani Mwanza kukagua ujenzi wa Vivuko Vitano ambavyo vinajengwa na Kampuni ya Songoro Marine Transport

Serikali imesema hadi kufikia mwezi Oktoba inatarajia kuingiza vivuko vipya vitano vyenye thamani ya zaidi ya Sh.milioni 28 katika Ziwa Victoria vinavyoendelea kutekelezwa ili kukabiliana na tatizo la usafiri na usafirishaji katika maeneo mbalimbbali ya Ziwa hilo.

Hayo yamebainishwa leo Mei 2,2025 na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa, wakati wa ziara na waandishi wa habari kutoka Mwanza na Shinyanga kwenye Karakana ya Ujenzi wa Vivuko Songoro Marine Transport ya jijini Mwanza.

Msigwa amesema, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan,amedhamilia kutatua kero ya usafiri na usafirishaji wa majini, na kuamua kutoa fedha ili kujenga vivuko,vikiwamo vitano ambavyo vinajengwa Jijini Mwanza.

"Rais Samia huwa anaumia sana akiona wananchi wanapata shida ya usafiri na hata kupanda Mitumbwi, na kuna tukio moja aliona wanafunzi wanasaidizana kupanda kwenye Mtumbwi aliumia sana,"amesema Msigwa.

"Kazi kama hizi za ujenzi wa vivuko vipya inafanyika pia katika Ziwa Tanganyika na Nyasa, lengo ni kutatua changamoto ya usafiri na usafirishaji wa majini,"ameongeza.

1


Ameipongeza pia Kampuni ambayo inajenga vivuko hivyo,na kwamba serikali ina dhamira ya dhati kuwawezesha wawekezaji wazawa.

"Kulinda wawekezaji wa ndani, ni kulinda uchumi wa Taifa na kuijenga nchi," amesema Msigwa.

Mkurugenzi wa Uendeshaji na ujenzi wa Vivuko kutoka (TEMESA) Mhandisi Lukombe King'ombe,amesema ujenzi wa Vivuko hivyo Vitano utakamilika Septemba mwaka huu, na gharama zake ni sh.bilioni 28.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Songoro Marine Transport Meja Songoro,amemshukuru Rais Samia kwa kuendelea kuwa amini wawekezaji Wazawa, na hata kuwapatia kazi pamoja na kutatua changamoto ya usafiri majini.

Amesema kwamba, vivuko hivyo wanavijenga kwa ubora unaotakiwa, na watavikamilisha kwa wakati.

2