Mahakama Kuu yashindwa kutoa hukumu dhidi ya Catic International

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 02:30 PM May 02 2025
Wakili wa Waziri mstaafu Edgar Majogo katika kesi ya madai iliyopo katika Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi jijini Dar es Salaam, Peter Madeleka akizungumza na waandishi (hawapo pichani), baada ya kesi hiyo kuahirishwa mbele ya Jaji Lusungu Hemed.
Picha: Mpigapicha Wetu
Wakili wa Waziri mstaafu Edgar Majogo katika kesi ya madai iliyopo katika Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi jijini Dar es Salaam, Peter Madeleka akizungumza na waandishi (hawapo pichani), baada ya kesi hiyo kuahirishwa mbele ya Jaji Lusungu Hemed.

Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi imeshindwa kutoa hukumu dhidi ya Kampuni ya Catic International Engineering Tanzania Ltd, inayokabiliwa na kesi ya kulipa fidia ya Dola za Marekani milioni 3 (sawa na zaidi ya Sh bilioni 7) kwa Waziri mstaafu Edgar Majogo, kutokana na hitilafu ya mtandao na kuharibika kwa kompyuta ya mahakama.

Kwa mujibu wa hati ya madai na ushahidi uliowasilishwa na upande wa mlalamikaji, Machi 1, 2008, Majogo na kampuni hiyo waliingia mkataba wa upangaji kuhusiana na kiwanja namba 7 kilichopo Oysterbay, Dar es Salaam, chenye usajili wa hati namba 100376.

Majogo, ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Ulinzi wakati wa Serikali ya Awamu ya Tatu, anailalamikia kampuni hiyo kwa kukiuka masharti ya mkataba waliokubaliana, kuhusu ujenzi na umiliki wa jengo hilo kwa ubia wa muda fulani.

Akiahirisha usomaji wa hukumu hiyo, Jaji Lusungu Hemed alisema:

“Kuliko kuwaweka hapa ni bora tupange siku nyingine ambayo tutataarifiana kwa sababu kompyuta ime-collapse, hatuwezi kuendelea,” alisema Jaji Hemed.

Baada ya kauli hiyo, mawakili wa pande zote walikubaliana na uamuzi wa kuahirisha, na walikubaliana kupanga tarehe nyingine ya kusomwa kwa hukumu hiyo.

Katika kesi hiyo, Majogo aliwakilishwa na Wakili Peter Madeleka, ambaye aliieleza mahakama kuwa kampuni hiyo ilikiuka masharti ya msingi ya mkataba waliouingia mwaka 2008. Madeleka aliiomba mahakama iamuru mteja wake alipwe Dola za Marekani milioni 2.88 kwa ukiukwaji wa kifungu cha 2(a), na Dola 120,000 kwa uvunjaji wa kifungu cha 1(b) cha mkataba huo.

Kwa mujibu wa kifungu cha 2(a) cha mkataba, Catic ilitakiwa kujenga jengo la ghorofa tatu lenye vyumba vya makazi 24 na ghorofa ya chini (basement), kwa gharama zake mwenyewe. Hata hivyo, ilidaiwa kuwa mdaiwa alijenga jengo hilo bila kujumuisha ghorofa ya chini, kinyume na masharti ya kifungu hicho pamoja na kifungu cha 4(f).

Majogo alidai kuwa kitendo hicho kimepunguza thamani ya kiuchumi ya kiwanja hicho, ambacho ni mali yake halali, hivyo kuathiri maslahi yake ya kimapato na uwekezaji.