Msajili ataka wananchi kuwa makini na AI, 'fake news'

By Salome Kitomari , Nipashe
Published at 10:39 AM May 03 2025
news
Salome Kitomari
Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania, Jaji Fransis Mutungi

Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania, Jaji Fransis Mutungi amewataka wananchi wawe makini na matumizi ya akili bandia au akili unde (AI), na habari za uongo ambazo zinalenga kusambaza propaganda na kupotosha umma.

Ameyasema hayo leo Mei 3,2025 wakati wa ufunguzi wa Kikao cha Msajili wa Vyama vya Siasa na wahariri wa vyombo vya habari kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, 

Jaji Mutungi amesema tukio la waraka feki wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), uliosambaa jana Mei 2, 2025 uliojitokeza ni mfano halisi wa habari potofu na kwamba ni muhimu kutafuta habari katika vyama vya kuamini,

“Vyama viwahimize wafusi wao kufuata sheria na taratibu kuwa na kukumbuka kuwa kuna maisha baada ya uchaguzi na kwamba amani ni msingi kwa nchi kila mmoja anawajibu wa kuilinda ikiwamo waandishi wa habari,”amesema.

Aidha, amesema wameanzisha program za kutoa elimu na lengo ni kila chama kuwa na maarifa sahihi ya kushiriki uchaguzi kwa njia ya amani ambazo zitaanza hivi karibuni.

Amesema wanashirikiana kwa karibu na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU, Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), ili vyama vipate taarifa za maadili, ulinzi wa data na uwajibikaji wakati wa uchaguzi, lengo ni kuwa na uchaguzi huru, wa haki na amani.

“Tunatoa wito kwa waandishi na wahriri kuripiti habari sahihi zisizoegemea upande wowote, tutatoa mafunzo kwa waandishi kuhusu sheria, ili kuhakikisha uchaguzi unakuwa kidemokrasia na wenye maadili,”amesema.

Aidha, amesema ni muhimu vijana na wanawake wanapata nafasi ya kushiriki mchakato wa uchaguzo iwe kwa kupiga kura kugombea au kushiriki midahalo, na kwamba vyombo vya habari vishiriki kutoa elimu hiyo.

Awali, akieleza madhumuni ya kikao hicho, Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania, Mohamed Ali Ahmed, amesema ni kipindi muhimu ambacho wanahabri wanachukua hatua muhimu kuhabarisha umma kuhusu uchaguzi na demokrasia nchini.

“Waandishi ni miongoni mwa wanaolifanya taifa kuwa na amani na uchaguzi, na ikiwa waandishi hawatatimiza wajibu vizuri vitasababisha nchi kuingia kwenye matatizo. Msajili ndiye mdai mkubwa wa kusimamia demokrasia nchini,”amesema.