Wakunga watoa maombi haya kwa serikali, wadau wa afya

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 12:53 PM May 03 2025
CHAMA cha Wakunga Tanzania (TAMA), kimeiomba serikali kuwapa motisha kama kichocheo cha kuwawezesha kufanya yao kwa ufanisi.
PICHA: MTANDAO
CHAMA cha Wakunga Tanzania (TAMA), kimeiomba serikali kuwapa motisha kama kichocheo cha kuwawezesha kufanya yao kwa ufanisi.

CHAMA cha Wakunga Tanzania (TAMA), kimeiomba serikali kuwapa motisha kama kichocheo cha kuwawezesha kufanya yao kwa ufanisi.

Ombi hilo limetolewa na rais wa chama hicho, Dk. Beatrice Mwilike jijini Dar es Salaam jana katika mdahalo uliohusu changaamoto za afya ya mama na mtoto ambazo wakunga wanakumbana nazo wakati wa majanga mbalimbali, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wakung Duniani itakayofikia kilele cha Mei 5 mwaka huu.
"Wakunga wanafanya kazi nzuri na ngumu, lakini suala la motisha limekuwa gumu, kwani mkunga ambaye amejiendeleza kielimu hadi kupata digrii ya uzamili, anapaswa alipwe au apate maslahi kulingana na kiwango chake cha elimu," amesema Dk. Beatrice.
Amesema hilo halifanyiki, na kwamba wakunga ni nguzo muhimu katika afya ya uzazi, hasa wakati wa migogoro na majanga ya asili au mabadiliko ya tabianchi.
Huduma zao haziwezi kuahirishwa na wanahitaji msaada wa kutosha ili kuendelea kutoa huduma zao, pia wanaweza kuchangia Kwa asilimia 90 ya kupunguza vifo vya mama na mtoto," amesema.
Aidha, ametoa wito kwa serikali na wadau wengine wa afya kuendelea kuwekeza kwa wakunga kwa kuwapa mafunzo, vifaa na mazingira bora ya kufanya kazi.
Mkurugenzi wa Idara ya Afya ya Mama na Mtoto kutoka Wizara ya Afya, Dk.Ahmad Hemed amesema serikali inathamini mchango wa wakunga kwenye afya ya uzazi, na kwamba inachukua hatua mbalimbali za kuboresha huduma zao, ikiwamo kuongeza ajira mpya kwa wahitimu wa ukunga kila mwaka ili kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma bora za uzazi katika vituo vya afya.
Mbali na hatua hiyo. ajira, amesema serikali imeboresha mafunzo kwa wakunga kwa vitendo na kuwapatia vifaa vya kisasa ili wafanye kazi katika mazingira salama.
Amesema serikali pia imeanzisha mifumo ya usimamizi na kufuatiliaji wa taaluma ya ukunga kwa ufafanuzi, Kwa lengo la kuhakikisha wakunga wanaendelea kupata mafunzo kazini na kusimamiwa kwa weledi ili huduma zinazotolewa ziwe salama na zenye utu.
"Wizara ya Afya inathamini mchango mkubwa wa wakunga katika kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto, inaendelea kuboresha huduma za ukunga katika maeneo mengi yakiwamo hayo matatu niliotaja," amesema Hemed.
Aidha, ametoa wito kwa jamii kushirikiana na wakunga, kwa kuwa kila mtu ana jukumu la kuhakikisha mwanamke anapata huduma ni salama za uzazi na mtoto anazaliwa katika mazingira salama yenye staha.