Mahitaji ya dharura MNH hufikia 200-500 kila saa 24

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 05:01 PM May 27 2025
Watoa huduma wa dharura wa MNH wakionesha huduma ya dharura kwa vitendo
Picha: MNH
Watoa huduma wa dharura wa MNH wakionesha huduma ya dharura kwa vitendo

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH), imesema inatoa huduma kwa wagonjwa wa dharura kati ya 200 hadi 500 (MNH) kila siku.

Mkuu wa Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Dharura na Ajali MUHAS, Dk. Said Kilindimo, aliyasema hayo leo, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Huduma za Dharura na Ajali Duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka Mei 27.

Amesema lengo  la maadhimisho hayo ni  kutambua mchango mkubwa wa watoa huduma hao ambao huhakikisha maisha yanaokolewa kila siku, alifafanua kuwa magonjwa ya dharura yamekuwa yakiongezeka kwa kasi nchini kutokana na ajali, maafa ya asili kama maporomoko na milipuko ya magonjwa kama ilivyoshuhudiwa wakati wa mlipuko wa Uviko-19 mwaka 2020/2021.

Amesema katika kipindi hicho, vitengo vya dharura vilikuwa mhimili mkuu wa kukabiliana na janga hilo kwa kuhakikisha watoa huduma na wananchi wanalindwa ipasavyo.

Kwa mujibu wa Dk. Kilindimo, mafanikio yameanza kuonekana tangu kuanzishwa kwa Idara ya Huduma za Dharura Muhimbili, vifo vya wagonjwa wanaofika  hospitalini kwa hali ya dharura vimepungua kwa asilimia 40, jambo lililoifanya serikali kuongeza uwekezaji mkubwa katika eneo hilo, ikiwamo kujenga hospitali za dharura katika kila mkoa na wilaya na kuongeza vifaatiba kama mashine za CT-Scan.

“Huduma hizi zinafanyika saa 24, usiku na mchana, kwa juhudi kubwa za watoa huduma walioko mstari wa mbele kuhakikisha kila mgonjwa anapokea matibabu stahiki kwa wakati,” amesema Dk. Kilindimo.

"MUHAS imekuwa kinara wa kuzalisha madaktari bingwa wa magonjwa ya dharura, hadi sasa zaidi ya madaktari 105 wamehitimu na kuanza kutoa huduma kote nchini. Hata hivyo, idadi hiyo bado haitoshelezi mahitaji ya sasa,” amesema.

Akizungumzia hali halisi ya huduma za dharura mikoani, Dk. Michael Kimario, Daktari Mkazi na Mwanafunzi wa Udaktari Bingwa wa Magonjwa ya Tiba ya Dharura na Ajali  MUHAS anayetoka Hospitali ya Bulongwa, Wilaya ya Makete mkoani  Njombe, amesema kuna tofauti kubwa kati ya huduma za dharura zinazotolewa Muhimbili na zile za mikoani.

Mgeni rasmi wa maadhimisho hayo, Dk. Julieth Magandi, akimwakilisha Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Mohammed Janabi, amesema serikali itaendelea kuboresha huduma hizo ili ziweze kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa wakati.

Shirika la Afya Duniani (WHO), linabainisha magonjwa ya dharura husababisha vifo vya watu takribani milioni 37.8 kila mwaka duniani kote. Takwimu za mwaka 2019 pekee zinaonesha kuwa vifo milioni 27.2 vilitokana na magonjwa ya dharura kama mshtuko wa moyo, ajali na kiharusi.