Maadhimisho ya siku ya utumishi wa umma mwaka 2025 yamepangwa kufanyika kuanzia Juni 16-23, 2025 ili kutambua mchango na umuhimu wa watumishi wa umma katika kuleta maendeleo ya taifa.
Akizungumza leo na waandishi wa habari jijini Dodoma, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Juma Mkomi, amesema maadhimisho hayo kitaifa yatafanyika viwanja vya Chinangali jijini humo.
Amesema maadhimisho hayo yataambatana na maonesho ya kuwezesha watumishi wa umma kutambua dira, dhima, malengo, programu, mikakati, mafanikio na changamoto zinazokabili utumishi wa umma.
“Kuhamasisha na kuwapa motisha watumishi wa umma waendelee na kazi yao nzuri ya ujenzi wa Taifa na kuendelea kuwa wabunifu ili kutatua changamoto mbalimbali katika jamii;Kupata mrejesho kutoka kwa wateja/wananchi na wadau wanaowahudumia na kuandaa Utumishi wa Umma ili uweze kukabiliana na changamoto mbalimbali kwa lengo la kuleta maendeleo siku za usoni,”amesema.
Ametaja faida watakazopata wananchi kuwa ni kufahamu wajibu wao na haki zao ili pindi wanapokosa haki zao waweze kujua namna ya kuzipata.
Pia, amesema taasisi za umma kupata fursa ya kubadilishana uzoefu juu ya mbinu na mikakati mipya ya namna ya kutoa huduma bora kwa umma.
“Aidha, katika maonesho hayo, huduma mbalimbali zitatolewa papo kwa hapo ikiwemo vyeti vya kuzaliwa, vitambulisho vya taifa (NIDA), hati za viwanja, kupima afya kutoka Hospitali za Benjamin Mkapa, Taasisi ya Jakaya Mrisho Kikwete (JKCI), Muhimbili na Taasisi ya Mifupa (MOI). Vile vile kutakuwepo na huduma ya Gazeti la Serikali,”amesema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED