Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimefanya mabadiliko muhimu ya Katiba yake ya Januari 1977, kwa lengo la kuendana na kasi ya maendeleo ya teknolojia na mahitaji ya sasa ya uendeshaji wa chama. Mabadiliko hayo yamepitishwa rasmi katika Mkutano Mkuu Maalum wa CCM uliofanyika jijini Dodoma, yakilenga kuboresha mifumo ya utendaji na usimamizi wa rasilimali za chama.
Miongoni mwa mabadiliko hayo ni kuingizwa rasmi kwa utaratibu wa mikutano ya mtandao (E-Meeting) katika Katiba ya chama, kwa ngazi zote kuanzia wilaya hadi Mkutano Mkuu wa Taifa. Lengo kuu ni kurahisisha utendaji, kuongeza ufanisi, na kupunguza gharama, hususan katika nyakati za dharura.
Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa CCM Taifa,Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa chama kimeamua kuendana na kasi ya dunia ya kidijitali ili kuboresha mifumo ya mawasiliano na uendeshaji wa shughuli zake.
"Chama chetu kinaenda dunia inavyokwenda. Leo ndani ya chama tunafanya kazi kidigitali. Tumeweka mitambo ya mawasiliano itakayorahisisha kuwasiliana na mikoa pamoja na wilaya. Tumeanzisha wazo la E-Meeting kwa vikao vya sekretarieti ya wilaya, kamati za siasa, kamati maalum za Halmashauri Kuu, Kamati Kuu ya chama, na Mkutano Mkuu wa Taifa,” amesema Samia.
Amefafanua kuwa vikao hivyo vya mtandao vitafanyika pale tu inapokuwa na ulazima na kwa idhini ya Katibu Mkuu wa CCM, huku akisisitiza kuwa hatua hiyo inalenga kuepusha matumizi mabaya ya mifumo ya kidijitali ndani ya chama.
Katika hatua nyingine, Katiba ya CCM imefanyiwa marekebisho kuhusiana na usimamizi wa miradi ya chama inayotekelezwa katika ngazi za wilaya na mikoa. Sasa, miradi yote italazimika kupata idhini ya maandishi kutoka Baraza la Wadhamini kabla ya kutekelezwa, tofauti na utaratibu wa awali ambapo maamuzi yalifanyika katika ngazi husika.
“Katiba ya sasa inasema Bodi ya Wadhamini itakasimu madaraka yake kwa kamati za siasa za wilaya na mikoa, na wamekuwa wakiendelea kutekeleza miradi hiyo. Hata hivyo, sasa tunaongeza kipengele cha ‘kwa maandishi’ ili kuwe na uthibitisho rasmi wa idhini hiyo,” ameeleza Samia.
Aidha, Katiba ya CCM imefanyiwa marekebisho kuongeza idadi ya wajumbe wa Baraza la Wadhamini kutoka wanane (8) hadi tisa (9). Mabadiliko hayo yanalenga kufanikisha utekelezaji wa matakwa ya Sheria ya Vyama vya Siasa, ambayo inataka idadi isiyogawanyika kwa mbili kwa mujibu wa taratibu za kisheria.
"Sheria ya Vyama vya Siasa inahitaji idadi isiyogawanyika kwa mbili. Sasa tuna nane, tumeongeza mmoja ili kufikia tisa. Hii inaleta uwiano na kuifanya bodi hiyo kuwa na nguvu zaidi katika kusimamia mali na miradi ya chama," amefafanua.
Mabadiliko mengine muhimu ni katika eneo la uchumi wa kisiasa wa chama, ambapo Baraza la Wadhamini litakuwa na mamlaka ya kutoa ushauri wa kitaalamu kwa maandishi kuhusu namna ya kuongeza tija katika miradi ya chama, sambamba na kuelekeza nguvu kubwa kwenye kampuni za chama.
Hatua hii inalenga kuongeza ufanisi katika usimamizi wa mali na miradi ya CCM kwa kuhakikisha kuwa maamuzi yote yanazingatia utaalamu, uwazi, na misingi ya utawala bora.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED