Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mobhare Matinyi, amewataka Watanzania wanaoishi nje ya nchi (Diaspora) kujenga umoja na ushirikiano miongoni mwao popote walipo duniani, huku wakipigania maslahi ya taifa lao wakati wote.
Balozi Matinyi alitoa wito huo alipokutana na Watanzania wanaoishi nchini humo, katika kikao kilichofanyika katika viwanja vya Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania jijini Stockholm. Kikao hicho kililenga kujenga mahusiano na kuimarisha mawasiliano baina ya ubalozi na jumuiya ya Watanzania, sambamba na kujadili masuala muhimu yanayohusu Diaspora.
Akizungumza katika kikao hicho, Balozi Matinyi alifafanua tafsiri ya neno "Diaspora" kwa mujibu wa Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania ya mwaka 2001, toleo jipya la mwaka 2024, iliyozinduliwa rasmi tarehe 19 Mei 2025 jijini Dar es Salaam na Rais Samia Suluhu Hassan.
“Kwa mujibu wa sera hiyo, 'Diaspora' wanajumuisha raia wa Tanzania wanaoishi nje ya nchi (Citizen Diaspora) pamoja na raia wa mataifa mengine wenye asili ya Kitanzania (Non-Citizen Diaspora),” alieleza Balozi Matinyi.
Aidha, aliwahimiza Watanzania hao kutoka miji mbalimbali ya Sweden kushiriki kikamilifu katika juhudi za maendeleo ya taifa, hususan kupitia uwekezaji nchini, akirejea kauli ya Rais Samia inayosisitiza mchango wa Diaspora katika uchumi wa taifa.
Balozi Matinyi alisisitiza kuwa mchango huo wa Diaspora ni ushahidi wa dhamira ya Watanzania walio nje katika kuchangia ustawi wa jamii na maendeleo ya taifa lao, akiahidi kuendelea kushirikiana nao kwa karibu kupitia ubalozi huo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED