Katika kuunga mkono huduma za afya kwa mama na mtoto pamoja na huduma za dharura, Klabu ya The Runners kwa kushirikiana na Ups Dar City Marathon wamekabidhi vifaa tiba muhimu katika Hospitali ya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Makabidhiano hayo yalifanyika Mei 30, 2025 katika Hospitali ya Mnazi Mmoja ikiwa ni sehemu ya faida iliyopatikana kupitia mbio za Ups Dar City Marathon zilizoshirikisha zaidi ya washiriki 3,500 zikiwa na lengo la kusaidia jamii kwa vitendo.
Makamu wa Rais wa Klabu ya The Runners, Godfrey Mwangungulu, ambaye pia ni Msemaji wa mbio hizo, amesema kuwa mara baada ya kusherehekea mafanikio ya mbio hizo, waliamua kuirejeshea jamii kwa kutoa msaada wa vifaa vinavyosaidia huduma za mama na mtoto pamoja na huduma za dharura.
“Mahitaji ya afya kwa kina mama wajawazito na watoto wachanga ni makubwa, tunatoa wito kwa jamii kushirikiana kwa pamoja katika kusaidia sekta ya afya, kwani kila mchango unaokoa maisha,” amesema Mwangungulu.
Kwa upande wake, Meneja wa Huduma Endelevu na Matukio kutoka Benki ya Absa, Abigael Lukuvu, ameema kuwa huu ni mwaka wa tatu benki hiyo kudhamini mbio hizo, na wanajivunia kuwa sehemu ya kugusa maisha ya Watanzania kupitia ushiriki wao.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mnazi Mmoja, Dk. Linda Mtasa, alishukuru kwa msaada huo na kueleza kuwa vifaa hivyo vitasaidia kwa kiasi kikubwa katika utoaji wa huduma bora, hasa kwa watoto wachanga na wanawake wajawazito.
“Tumepokea kifaa cha kisasa cha kupima mapigo ya moyo ya mtoto tumboni, ambacho kina uwezo wa kutoa majibu kwa usahihi wa asilimia 100. Pia tumepewa visaidizi vya oksijeni kwa ajili ya dharura, ambavyo vitasaidia kwa kiwango kikubwa kuokoa maisha,” amesema Dk. Mtasa.
Ameongeza kuwa “ Klabu ya The Runners imekuwa mstari wa mbele kila mwaka kusaidia hospitali hiyo kwa vifaa mbalimbali, na safari hii wamepokea pia seti maalum kwa ajili ya watoto wachanga. “Tutavitumia vifaa hivi kwa malengo yaliyokusudiwa ili kulinda afya ya mama na mtoto,”amesema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED