Tanzania yataka vijana watumie Intaneti kwa manufaa

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 12:55 PM May 31 2025
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa
PICHA: MPIGAPICHA WETU
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa

Tanzania imesema iko tayari kushiriki katika uchumi wa kidijitaji na kutimiza malengo ya milenia ya mageuzi ya teknolojia yaliyopo duniani, na kuhamasisha vijana watumie intaneti kwa manufaa.

Akizundua kongamano la 14 la Jukwaa la Utawala wa Mtandao Afrika (AfIGF) Jana kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,Dk Dotto Biteko, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa amesema Tanzania iko tayari tayari kishiriki katika mageuzi hayo ya Intaneti.

Katika hili lililojumuisha viongozi mbalimbali kutoka Bara hilo, wamejadili mambo mbalimbali ikiwamo jinsi ya kutumia intaneti kuinua zaidi Afrika, lakini pia kuwainua vijana wa bara hilo hasa katika kipindi hiki cha ukosefu wa ajira na kwamba huo unaweza kuwa mwarobaini wa vijana kutafuta fursa za masoko.

Silaa amesema idadi kubwa inayoongoza kwa matumizi ya Intaneti  katika nchi mbalimbali za Afrika ni vijana, akiwaasa watumie katika njia sahihi wasitumie katika maudhui yasiyofaa, bali katika kukuza uchumi wa kidigitali na kutafuta mbinu mbalimbali za masoko.

Amesema katika kuhakikisha Tanzania inatumia mtandao kwa manufaa, kumekuwa na mageuzi mbalimbali ya kidijitali nchini. "Mfano serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kwa sasa imeendelea kufanya mageuzi mbalimbali ya kidijitali ikiwemo kuanzishwa masomo ya ubunifu, kuanzia shule za elimu ya awali mpaka elimu ya juu lengo lake ikiwa kuchochea mageuzi ya kidijitali," amesema.

Pia amesema kwa sasa mtandao ni muhimu katika utoaji wa huduma mbalimbali ikiwemo maji, nishati ya umeme na nyinginezo na ndiyo maana Serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti katika mageuzi ya kidijitali.

Silaa amesema serikali imeendelea kuhamasisha na kuboresha mazingira ya kidijitali mijini na vijijini. Amesema jukwaa hilo ni muhimu kwa maendeleo ya teknolojia afrika na dunia kwa ujumla, hivyo Tanzania kuandaa mtandao huu ni sehemu ya juhudi za kuendelea kuchochea mageuzi ya kidijitali.

Kwamba, matumizi ya intaneti kwa wanawake na wanaume kwa mjini na vijijini, yamepanda hivyo lazima juhudi ziongezwe ili kuongeza matumizi hayo hasa maeneo ya vijijini. "Kwa kuliona hili, Tanzania pia tumewekeza zaidi vituo vya Tehama ambavyo vitaibua fursa za mafunzo kwa vijana na kupitia hivyo vituo vijana watajua intaneti, namna ya kuitumia. Kwa sasa Tanzania ina vituo nane ambavyo vipo chini ya Tume ya Tehama, kwa ajili ya kuwanoa vijana kidijitali," amesema Silaa.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mohammed Hamis Abdulla amesema jitihada kubwa zimefanyika katika kukuza dijitali nchini, ikiwemo kuhamasisha uchumi wa kidijitali, serikali imefanya jitihada kubwa. "Mapinduzi ya kidijitali yana umuhimu mkubwa katika jamii ya Afrika ambayo yanaambatana na athari mbalimbali ikiwemo uhalifu wa mitandaoni, hivyo ndiyo maana tunaungana pamoja kuona namna ya kuhamasisha usalama," amesema.

Amesema kuwa mkutano huo utaandaa Afrika ya baadae ambayo inatakiwa kuwa na maendeleo makubwa ya uchumi wa kidijitali, na ili kufika huko ni lazima iungane katika kuchochea mageuzi hayo. Mwenyekiti wa Jukwaa la Mtandao wa AfIGF, Alhagie Mbow amedadavua kauli mbiu isemayo kuelekeza mustakabali wa kidijitali wa Afrika kwa utawala jumuishi, ustahimilivu, ubunifu na usawa.

Amesema hiyo ni kauli mbiu ambayo ina taswira ya hali halisi kwa Afrika, hivyo inatakiwa kuchukua hatua, inadhihirisha kwamba kwa sasa Afrika si mtazamaji tena wa mtandao kiwango kilikuwa chini lakini kwa sasa ni mtendaji.

"Kwa hali ilivyo kwa sasa uchumi wa kidijitali unaokua kwa kasi unawalenga zaidi vijana, lakini bado kuna pengo la usawa kati ya mwanamke na mwanaume hiyo pia ni changamoto, lakini changamoto nyingine ni miundombinu bado kuna maeneo haijafika," ameeleza na kuongeza; "Pia kuna makundi ya vijana yaliyotengwa ambayo hayafikiwi na hiyo huduma."