Kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwake mwaka 2019, Hospitali ya Serikali ya Wilaya ya Songea Vijijini, iliyopo kata ya Mpitimbi, mkoani Ruvuma, imefanikiwa kufanya upasuaji wa mifupa chini ya uangalizi wa madaktari bingwa – hatua ambayo imeweka historia mpya katika utoaji wa huduma za afya kwa wananchi wa eneo hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari, Dk. Adam Ngunga, Mratibu wa Huduma za Tiba katika halmashauri hiyo, amesema mafanikio hayo ni matokeo ya ujio wa madaktari bingwa na bingwa bobezi waliowasili kupitia mpango wa serikali.
“Hii ni hatua kubwa kwa mara ya kwanza tumefanikisha upasuaji wa mifupa hapa Mpitimbi, bila kumpeleka mgonjwa Songea Mjini au Mbeya. Tunaishukuru sana Serikali kwa kutuletea madaktari bingwa na vifaa tiba vya kisasa,” amesema Dk. Ngunga, ambaye alimwakilisha Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo, Dk. Kihaule.
Dk. Ngunga ameongeza kuwa hatua hiyo si tu imepunguza gharama na usumbufu kwa wagonjwa, bali pia imeimarisha imani ya wananchi kwa huduma zinazotolewa na hospitali ya wilaya.
Upasuaji huo ni sehemu ya mkakati wa Wizara ya Afya chini ya serikali ya awamu ya sita, wa kuhakikisha huduma za kibingwa na bobezi zinawafikia wananchi hadi vijijini, kama inavyoainishwa kwenye Dira ya Maendeleo ya Taifa.
Kwa sasa, hospitali hiyo inaendelea kupata maboresho ya miundombinu na vifaa tiba, ikiwa ni pamoja na mafunzo kwa wataalamu wa afya waliopo, ili kuhakikisha huduma hizo zinaendelea kutolewa kwa ufanisi na uendelevu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED