MBUNGE wa Jimbo la Makambako, Deo Sanga (Jah People) anatarajiwa kufikishwa mbele ya Kamati ya Maadili ya Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Makambako Wilayani Njombe, kufuatia tuhuma za kutoa taarifa za uongo kwa wananchi.
Sanga anatuhumiwa kujinasibu hadharani kuwa ndiye aliyegharamia safari ya madiwani kwenda kujifunza katika Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, hali ambayo imeelezwa si ya kweli, kwani gharama zote za safari hiyo zilitolewa na halmashauri hiyo.
Hayo yameibuka leo katika wa kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani kilichofanyika mjini Makambako kwa ajili ya tathmini ya utekelezaji wa miradi kwa kipindi cha robo ya tatu. Baadhi ya madiwani akiwemo Diwani wa Kata ya Kitandililo, Imani Fute, alihoji chanzo cha fedha hizo, akieleza wasiwasi wake juu ya taarifa za mbunge huyo kuutangazia wananchi kwamba ndiye aliyefanikisha safari hiyo huku Diwani wa kata ya Kivavi Alimwimike Sahwi ameomba Mjumbe huyo afikishwe kamati ya maadili ili kujibu tuhuma hizo.
Mara baada ya madiwani kuhoji, Mwenyekiti Halmashauri ya mji wa Makambako Hanana Mfikwa amesema kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi Eliud Mwakibombaki fedha iliyotumika kuwapeleka Kahama ni ya halmashauri hivyo mjumbe alitoa taarifa ya uongo hivyo kwa kuzingatia kanuni na taratibu atafikishwa kwenye kamati ya maadili kuhojiwa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED