WATUMISHI wa dini kutoka madhehebu mbalimbali, wakiongozwa na Mchungaji Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Ushirika wa Njombe mjini Nelson Godiwe, wameungana kwa pamoja katika ibada maalum ya kuwaombea watumishi wa Halmashauri ya Mji Njombe.
kizungumza katika ibada iliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri hiyo, Mchungaji Godiwe amesema kuwa sala na dua ni nguzo muhimu katika kuhakikisha mazingira ya kazi yanabaki kuwa ya utulivu na yenye maadili ambapo alisisitiza kuwa viongozi wa umma wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuomba baraka za Mungu kwa ajili ya kazi zao.
Kwa upande wake, Shehe wa mkoa wa Njombe, Rajabu Msigwa amesema kuwa mafanikio ya taifa lolote yanatokana na mshikamano na upendo miongoni mwa wananchi wake ambapo ushirikiano kati ya viongozi wa serikali na wananchi unapaswa kuimarishwa kupitia misingi ya heshima na maadili ya kidini.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe, Kuruthum Sadick amesema kuwa ni wajibu wa kila mtumishi wa umma kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na moyo wa kujitolea, kwa kuwa wanahudumia wananchi na taifa kwa ujumla.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED