Katika jitihada za kuimarisha mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini, wananchi wa Kijiji cha Heikonti kilichopo Kata ya Tae, Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, wamejitokeza kwa hiari kung’oa visiki vya mirungi zao haramu linalotumika kama dawa ya kulevya ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa operesheni ya kuondoa kabisa kilimo cha mirungi katika eneo hilo.
Ofisa Elimu Kanda ya Kaskazini wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Shaban Miraji, ambaye alithibitisha kuwa zoezi hilo limefanyika kwa mafanikio makubwa kwa kushirikiana na Serikali ya Wilaya ya Same pamoja na wananchi wenyewe.
"Ni hatua ya kihistoria kuona wananchi wa Heikonti wakijitokeza kwa hiari kung’oa visiki vya mirungi, jambo linalothibitisha kwamba elimu dhidi ya kilimo cha dawa za kulevya inaendelea kuzaa matunda chanya," amesema Miraji.
Miraji anasema hamasa hii ya wananchi imechangiwa kwa kiasi kikubwa na elimu iliyotolewa na mamlaka mbalimbali za Serikali, ikiwemo DCEA yenyewe, kuhusu madhara ya mirungi na faida ya kuachana na kilimo hicho. Serikali imekwishaandaa mbadala wa mazao zaidi ya nane kwa ajili ya wanakijiji wa Kata ya Tae, Vudee na maeneo mengine yaliyokuwa na historia ya kilimo cha mirungi.
Zoezi hili la kung’oa visiki linatokana na operesheni kubwa ya kitaifa ya uteketezaji wa mashamba ya mirungi iliyofanyika mwezi Machi 2025, chini ya usimamizi wa Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas James Lyimo, katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Same.
Kwa mujibu wa Miraji, hatua hii ya wananchi kushiriki moja kwa moja katika uondoaji wa visiki inadhihirisha dhamira ya kweli ya kutokomeza kabisa mirungi katika maeneo ya milima ya Same, ambapo awali kilimo hicho kilikuwa sehemu ya maisha ya kila siku.
“Tunashukuru kuona mabadiliko ya fikra kwa jamii hizi, kwani hatua ya kung’oa visiki kwa hiari si tu kwamba ni ishara ya ushirikiano baina ya Serikali na wananchi, bali pia ni ushahidi wa kuanza kuachana na utegemezi wa zao la mirungi,” amesema Miraji
Aidha, DCEA kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), wameendesha elimu kinga kwa wanafunzi zaidi ya 350 wa Shule ya Sekondari ya Tae kwa lengo la kuwajengea uelewa wa athari za dawa za kulevya na umuhimu wa kuzipiga vita.
Katika mafunzo hayo, wanafunzi walihamasishwa kuwa mabalozi wa mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa kushirikiana na mamlaka kwa kutoa taarifa kupitia namba ya bure 119 endapo watabaini kuwepo kwa dalili zozote za uhalifu wa dawa hizo katika jamii zao.
DCEA imesisitiza kuwa mapambano dhidi ya dawa za kulevya si ya serikali peke yake, bali ni jukumu la kila Mtanzania. Kwa msingi huo, wananchi wote wanaaswa kushiriki kikamilifu katika kutokomeza matumizi na biashara ya dawa za kulevya, hasa kwa kutoa taarifa kwa vyombo husika na kuachana na shughuli zote zinazohusiana na kilimo haramu kama cha mirungi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED