Kampuni ya Egcore, inayojihusisha na shughuli mbalimbali za kijamii, imejitokeza kusaidia ujenzi wa choo kwa ajili ya walimu wa Shule ya Msingi Shikizi Gongoni, iliyopo kata ya Zinga, wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ukaguzi wa mradi huo, Mkurugenzi wa Egcore, Hassan Kashingo, alisema uamuzi wa kujenga choo hicho umetokana na taarifa walizopokea kuhusu walimu na wanafunzi kutumia choo kimoja, hali iliyokuwa ikileta usumbufu na changamoto za kiafya.
“Kwa sasa choo hicho kipo katika hatua ya umaliziaji na lengo ni kuhakikisha walimu wanapata mazingira bora ya kufanyia kazi bila usumbufu,” alisema Kashingo.
Mbali na ujenzi wa choo hicho, Kashingo alibainisha kuwa kampuni hiyo ina mpango wa kujenga darasa moja kwa ajili ya shule hiyo mara baada ya kukamilisha choo, ili kuandaa mazingira kwa ajili ya ongezeko la wanafunzi mwaka ujao.
Kwa mujibu wa Kashingo, kampuni hiyo tayari imetoa msaada wa matofali na saruji kwa ajili ya Shule ya Msingi Zinga pamoja na kusaidia vituo vya afya na vya kulelea watoto katika kata hiyo.
“Kampuni yetu imejikita kusaidia jamii. Tutaendelea kushirikiana na Serikali na wananchi kuhakikisha watoto hawakosi huduma muhimu, hasa katika kituo cha kulelea watoto kilichopo hapa Zinga,” alisisitiza Kashingo.
Pamoja na shughuli za kijamii, Egcore pia imeanzisha kituo cha kuoshea magari, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuwawezesha vijana kupata ajira na kujitegemea kiuchumi.
Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule Shikizi Gongoni, Lidya Lucas, ameishukuru kampuni hiyo kwa msaada huo mkubwa na kuomba waendelee kusaidia ujenzi wa vyumba vya madarasa ili shule hiyo iweze kutoa elimu bora kwa wanafunzi wote.
“Tuna matumaini kwamba shule yetu ikisajiliwa rasmi, wanafunzi wetu wataweza kufanya mitihani ya kitaifa hapa hapa, badala ya kwenda shule mama umbali wa kilomita tano,” alisema Lidya.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Gongoni, Susana Kazimoto, pia ameipongeza kampuni ya Egcore kwa namna inavyoendelea kushirikiana na Serikali katika kuleta maendeleo ya kijamii, hasa katika sekta ya elimu na afya.
Kampuni ya Egcore, yenye makao yake makuu Same, mkoa wa Kilimanjaro, imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali ya kijamii katika mikoa ya Kilimanjaro na Tanga, ikiwemo Halmashauri ya Handeni.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED