Mauaji ya wanandoa Moshi yazua jambo

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 02:29 PM May 30 2025
Geofrey Anael Mota (60) na Blandina Felix Ngowi (53)
Picha: Mpigapicha Wetu
Geofrey Anael Mota (60) na Blandina Felix Ngowi (53)

Mauaji ya wanandoa, Geofrey Anael Mota (60) na Blandina Felix Ngowi (53), wakazi wa Mtaa wa Msufini, Kata ya Msaranga katika Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, yameibua gumzo baada ya kuuawa na watu wasiojulikana.

Wanandoa hao waliokuwa katika makazi yao ya kupanga, wamekutwa baba akiwa ameuawa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali shingoni, na mkewe mwili wake haujakutwa na majeraha.

Akizungumzia tukio hilo leo, Mei 30, 2025, Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP), Simon Maigwa, amesema wanandoa hao wamekutwa wakiwa nyumbani kwao wameuawa tarehe 29/2025 majira ya saa 1:30 usiku.

Alisema kuwa Jeshi hilo, linawasaka watu waliohusika katika mauaji ya watu wawili, ambao ni mke na mumewe.

"Tukio hilo limetokea ndani ya nyumba ya kupanga waliokuwa wakiishi wanandoa hao pamoja na kijana wao wa kiume (jina limehifadhiwa) ambaye ametoweka baada ya mauaji hayo kutokea.”

Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo cha tukio hilo na kuwakamata wote waliohusika na mauaji hayo.

Kwa mujibu wa Kamanda Maigwa, miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufani ya Kanda ya Kaskazini ya KCMC kwa uchunguzi na taratibu nyingine.