Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga imeanzisha rasmi huduma za matibabu ya kibingwa ya macho, ikiwa ni hatua kubwa katika kuboresha huduma za afya kwa wakazi wa mkoa huo na maeneo jirani. Huduma hizo zitaanza kutolewa rasmi Juni 2, 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 30, 2025, Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. John Luzila, amesema kuwa siku ya uzinduzi wa huduma hiyo itaambatana na “camp” maalum ya macho kwa wananchi, itakayodumu kwa siku tano kuanzia Juni 2 hadi Juni 6, 2025. Baada ya hapo, huduma hizo zitaendelea kutolewa mara mbili kwa wiki.
“Tumeanzisha rasmi huduma za kibingwa za macho hapa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga. Huduma zitaanza Juni 2, na tumejipanga kuhakikisha wananchi wanapata matibabu bora, karibu na maeneo yao,” amesema Dk. Luzila.
Amefafanua kuwa hospitali tayari ina daktari bingwa wa macho ambaye alipelekwa masomoni na sasa amerudi kutoa huduma, sambamba na ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa vyenye thamani ya shilingi milioni 79.
Huduma zitakazotolewa katika Kliniki ya Macho ni pamoja na:
📌Uchunguzi wa kina wa macho
📌Matibabu ya mtoto wa jicho
📌Matibabu ya presha ya macho
📌Matibabu ya aleji ya macho
Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wa Shinyanga wameipongeza hospitali hiyo kwa kuanzisha huduma hizo. Yohana Shija, mkazi wa Shinyanga, alisema huduma hiyo itawaondolea usumbufu wa kusafiri umbali mrefu kutafuta matibabu ya macho.
“Tulikuwa tunasafiri hadi Bugando au Muhimbili kufuata madaktari bingwa wa macho, lakini sasa huduma hizi zote zitapatikana hapa hapa Shinyanga,” amesema Janeth Kalikale, mkazi mwingine wa mkoa huo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED