Mkurugenzi wa Taasisi ya Shujaa Cancer Foundation, ambaye pia amepona saratani ya titi, Glory Kida, ameikumbusha jamii kwamba ugonjwa huo unatibika hospitalini.
Aidha, amesema taarifa zisizo sahihi zimekwamisha wagonjwa wa saratani kupata tiba kwa wakati, jambo linalosababisha wanachelewa kupata matibabu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya siku ya mashujaa wa saratani Dar es Salaam, Kida alisema amepona ugonjwa huo miaka 14 iliyopita, akieleza kuwa lengo la kuanzishwa kwa taasisi hiyo ni kuwajengea uwezo watu waliopona saratani, ili warejee kwenye maisha ya kawaida.
“Tumejikita kuwa sauti ya mashujaa, ili kusherehekea maisha. Kwa watu waliopita kwenye changamoto ya saratani siyo safari nyepesi, watu wengi wakiona umepata saratani wanaona ni kifo, sisi tunaamini kifo kimeandikwa kwa kila mtu, utaondoka kwa ugonjwa gani hatujui,” anasema.
Alifafanua kupata saratani sio kifo kwa kuwa wapo watu waliopona ugonjwa huo na wanaishi zaidi ya miaka 20.
“Watu wengi wanaogopa saratani na kusema kweli tiba yake sio nyepesi, sio rahisi, ni ghali; lakini mgonjwa aliyebainika katika hatua za awali, akipata tiba na kukamilisha dozi kikamilifu anapona kabisa,” alisema.
Bingwa wa ugonjwa huo katika hospitali ya Besta, Dk. Ndibalema Yemela, alisema Tanzania imepiga hatua kubwa kwenye matibabu ya saratani, kutokana na kufunga vifaa tiba vya kisasa na mifumo ya kiteknolojia inayorahisisha uchunguzi na tiba.
“Kuna habari ambazo sio nzuri kuhusiana na matibabu ya saratani. Wengine wanaamini wakianza tiba ndio wanapoteza maisha, vitu ambavyo sio kweli. Matibabu ya saratani yanayotolewa hospitalini yanaponesha hasa pale ugonjwa unagundulika mapema,” alisema.
Dk. Yemela anasema maadhimisho ya mashujaa wa ugonjwa huo, hufanyika kuikumbusha jamii kwamba maradhi hayo yanatibika na watu wanaendelea na maisha baada ya kukamilisha matibabu.
Katika maadhimisho ya siku ya mashujaa wa saratani, waliopona ugonjwa huo watafanya matembezi ya hisani yatakayoanzia Taasisi ya Ocean Road (ORCI), yatakayochangia huduma za matibabu kwa wagonjwa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED