Mkakati wa mawasiliano nishati safi kupikia kuzinduliwa Jumatatu

By Frank Monyo , Nipashe
Published at 05:27 PM May 30 2025
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba akizungumza na waandishi wa habari.
Picha: Mpigapicha Wetu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba akizungumza na waandishi wa habari.

Serikali kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU), Shirika la Maendeleo la Mitaji la Umoja wa Mataifa (UNCDF) na wadau wa maendeleo, inatarajia kuzindua Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano kuhusu Nishati Safi ya Kupikia.

Kuzinduliwa kwa mkakati huo kutakwenda sambamba na uzinduzi wa Kampeni ya Kitaifa ya Uhamasishaji na Uelimishaji unatarajiwa kufanyika Juni 2, mwaka huu, mkoani Dodoma.

Hafla hiyo itahusisha zaidi ya washiriki 200 wakiwemo maofisa waandamizi kutoka serikali kuu na serikali za mitaa, washirika wa maendeleo, watoa huduma za nishati safi, watafiti, taasisi za kifedha, asasi za kiraia na vyombo vya habari.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba, alisema jana kuwa mkakati huo ni nyenzo muhimu katika mchakato wa matumizi ya nishati safi ya kupikia.

“Mkakati huu wa mawasiliano ni nyenzo muhimu katika mchakato wetu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia. Tumejipanga kuhakikisha kuwa ujumbe huu unamfikia kila Mtanzania, kutoka mijini hadi vijijini, ili wananchi wetu wawe na taarifa sahihi, vifaa vinavyofaa, na uamuzi wa busara wa kutumia nishati bora zaidia,” alisema

Hatua hiyo, alisema  inalenga kusaidia utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia wa Mwaka 2024–2034, ambao unalenga kufikia matumizi ya asilimia 80 ya nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034. 

Mkuu wa Ushirika wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Marc Stalmans.
Alisema uzinduzi huo umeandaliwa kuchochea msukumo wa kitaifa kuhusu uelewa wa nishati safi ya kupikia, mabadiliko ya tabia, na ushiriki wa jamii.

Zaidi ya asilimia 90 ya kaya nchini, alisema bado zinategemea nishati ya kuni na mkaa, hali inayochangia hatari za kiafya, uharibifu wa mazingira, na uzalishaji wa gesi chafuzi.

"Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano kuhusu Nishati Safi ya Kupikia unalenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu faida za nishati safi, kutangaza teknolojia na vyanzo vya nishati vinavyopatikana kama vile gesi ya kupikia (LPG), gesi asilia, majiko banifu, umeme, mkaa na kuni mbadala, bioethanoli na biogesi," alisema. 

Alisisitiza mkakati huo utawezesha mabadiliko ya tabia na kuhamasisha mahitaji ya nishati safi, kuwawezesha wananchi kufanya uamuzi sahihi wa matumizi ya nishati na kutoa nafasi kwa vyombo vya habari vya ndani na mitandao ya kijamii kuweza kusambaza ujumbe wa nishati safi.

Mkuu wa Ushirika wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Marc Stalmans, alisema uelewa wa umma ni jambo la msingi katika kubadili mitazamo na kuleta suluhisho endelevu. Umoja wa Ulaya unajivunia kusaidia kampeni hii ya kitaifa, ambayo inaleta nishati safi katika mjadala wa kitaifa na kuifanya iweze kufikika kwa familia zote nchini.

Mtaalamu Mwandamizi wa Fedha kutoka UNDF, Immanuel Muro, alisema: “Tukiwa kama watekelezaji wa mpango huu, tumejizatiti kushirikiana na wadau mbalimbali hususan vyombo vya habari, jamii, mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO) na hata mashirika ya kidini (FBO) kuhakikisha uelewa sahihi na mabadiliko ya tabia kuhusiana na matumizi ya nishati safi ya kupikia.”

Mkakati huo unazinduliwa ikiwa ni mwaka mmoja tangu Raid Samia Suluhu Hassan, azindue Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia wa Mwaka 2024–2034, Mei 8, mwaka jana.

Lengo kuu la mkakati huo ni kuhakikisha matumizi ya nishati safi ya kupikia yanafikia asilimia 80 ya kaya ifikapo mwaka 2034.

Picha ya pamoja