Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Doroth Semu, ameomba ridhaa ya chama hicho ili kugombea urais katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari na wanachama wa chama hicho leo jijini Dar es Salaam, Semu alisema alichukua uamuzi huo baada ya kutathmini kwa kina hali ya sasa ya taifa na kuona haja ya kuwa na uongozi mpya, madhubuti, wenye dira na ulio na malengo ya kweli kwa maendeleo ya wananchi wote.
Akitaja vipaumbele vyake, amesema atajikita katika kujenga uchumi jumuishi, imara na unaostawi, utakaowawezesha Watanzania hasa vijana na wanawake, kupata ajira zenye kipato cha heshima.
Vipaumbele vyake ni:
- Kujenga Uchumi Jumuishi, Imara na Unaostawi
- ✍🏿Kuwekeza katika sekta zenye ajira nyingi kama kilimo, ufugaji, uvuvi na biashara ndogondogo.
- ✍🏿Kuimarisha mifumo ya biashara, ujasiriamali na upatikanaji wa mitaji kwa vijana na wanawake.
- ✍🏿Kuhuisha mifumo ya kodi na urasimishaji ili kuhamasisha biashara na ukuaji wa uchumi.
- ✍🏿Kutoa huduma bora za jamii kwa kila Mtanzania bila ubaguzi.
- ✍🏿Kuimarisha mfumo wa Hifadhi ya Jamii kwa wote, ukiwemo mfuko wa afya na pensheni ya taifa.
- Usimamizi Madhubuti wa Rasilimali za Taifa
- ✍🏿Kuweka sheria ya ushirikishwaji wa wananchi katika miradi ya uchimbaji wa rasilimali.
- ✍🏿Kuhakikisha rasilimali za taifa zinawanufaisha wananchi wa sasa na vizazi vijavyo.
- Mapambano Dhidi ya Rushwa, Uzembe na Ubadhirifu wa Mali za Umma
- ✍🏿Kuwajibisha wahusika wa ubadhirifu kulingana na taarifa za CAG.
- ✍🏿Kupambana na matumizi ya anasa ya viongozi, kupunguza matumizi yasiyo ya lazima.
- ✍🏿Kuelekeza fedha za umma kwenye huduma bora kwa wananchi na miradi ya maendeleo.
- Kuimarisha Demokrasia na Haki za Raia
- ✍🏿Kupigania uchaguzi huru na wa haki.
- ✍🏿Kulinda thamani ya kura ya kila Mtanzania.
- ✍🏿Kurejesha imani ya wananchi kwa taasisi za uchaguzi na mfumo wa demokrasia ya vyama vingi.
- ✍🏿Kuweka msingi wa taifa lenye mshikamano, haki, usawa na maendeleo ya watu wote.
“Tuna kazi moja kubwa — kuiondoa CCM madarakani na kuijenga Tanzania mpya kwa misingi ya haki, usawa, uongozi wa uwazi, na uchumi wa watu. Ndiyo dhamira yangu kuu.”