Serikali kusajili hati za kimila 52,000

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 05:49 PM May 29 2025
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Deogratius Ndejembi.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Deogratius Ndejembi.

Katika mwaka wa fedha 2025/26, Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imepanga kuandaa na kusajili Hati za Hakimiliki za Kimila 520,000, Hatimiliki 500,000, Vyeti vya Ardhi ya kijiji 100 na Hati za Sehemu ya Jengo 1,000.

Vilevile, miamala ya hatimiliki na nyaraka za kisheria 100,000 zitasajiliwa.

Ili kufikia lengo la utoaji wa Hatimiliki katika mwaka 2025/26, Wizara itaendelea kusambaza Mfumo wa e-Ardhi katika Halmashauri mbalimbali nchini ili kurahisisha na kuongeza kasi ya umilikishaji ardhi, kuendelea kuhimiza wananchi kuchangia gharama za urasimishaji na umilikishaji ardhi, kuziwezesha Halmashauri kutekeleza Programu za Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi na kuendelea na Kliniki za ardhi ili kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Deogratius Ndejembi, amesema hayo leo bungeni jijini Dodoma, wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara  katika mwaka wa fedha 2025/2026.