Fanyeni ukaguzi kwa weledi bila kumwonea mchimbaji yoyote – Mhandisi Kamando

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:21 PM May 29 2025
Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Migodi na Mazingira, Mhandisi Hamisi  Kamando.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Migodi na Mazingira, Mhandisi Hamisi Kamando.

Wakaguzi wa Migodi ya Madini na Baruti wametakiwa kufanya kazi kwa weledi, kuongeza ufanisi na kufuata taratibu na sheria za nchi katika utoaji wa huduma.

Hayo yamesemwa leo Mei 29, 2025 na Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Migodi na Mazingira, Mhandisi Hamisi  Kamando jijini Mwanza  wakati akifunga kikao kazi cha siku mbili cha wakaguzi migodi na baruti ambacho kililenga kujengeana uwezo ikiwemo kufanya maboresho ya  Kanuni mbalimbali za madini na Sheria ya Baruti.

‘’Tusikubali kuyumba au kuyumbishwa na hatimaye kutolewa kwenye mstari, tuendelee kufuata misingi, weledi na maadili katika utendaji kazi kwa kuepuka rushwa na kushinda vishawishi   na tamaa nyinginezo,’’amesema Mhandisi Kamando na kuongeza,


“Nitoe rai, tunatakiwa kuwajibika kwa kuzingatia nidhamu, uaminifu, uwazi na kuongeza bidii kwenye kazi katika kuhakikisha kuwa Sekta ya Madini inaendelea kuwa na mchango mkubwa kwenye Pato la Taifa,"amesema.


 Aidha, Mhandisi Kamando amesema kuwa kikao hicho pia kimetoa mapendekezo ya maboresho ya Kanuni za Usalama, Afya na Utunzaji wa Mazingira kwasababu zimepitwa na wakati kwa kuwa  maboresho ya Sheria za Madini Sura ya 123 yalifanyika mwaka 2017 kwa mara ya kwanza na Kanuni husika hazijarekebishwa hadi hivi sasa.

“Kutokana na marekebisho ya Sheria ya Madini  ni vyema sasa tukafanya maboresho ya kanuni za usalama, afya na mazingira ili ziweze kwenda sawa na Sheria na hivyo, kuimarisha ufanisi wa kazi, lakini pia kuna Sheria ya baruti ya mwaka 1963 na kanuni zake za mwaka 1964 nazo tumeona tufanyie maboresho ili usimamizi wa baruti nchini uwe mzuri zaidi,”amesema Mhandisi Kamando.


Naye Mwanasheria Mwandamizi wa Tume ya Madini, Damian Kaseko akiwasilisha mapendekezo ya Sheria ya Baruti, Sura ya 45 ambayo ilitungwa mwaka 1963 ameeleza kuwa maboresho yanayopendekezwa yanalenga kuboresha vifungu mbali mbali ili kuleta ufanisi katika usimamizi wa utekelezaji wa sheria husika.

Kwa upande wake Siri Boga, akizungumza kwa niaba ya washiriki amesema kikao kazi hicho kimewajengea  uwezo wakaguzi wa madini huku wakipatiwa mbinu mpya ambazo wanapaswa kuzifuata  wakati wa ukaguzi.

Wakati huo huo Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa  Simiyu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa (RMOs), Maige Makolobela akizungumza amesema kikao hicho ni muhimu kwa wakaguzi kupata mafunzo ya pamoja, kubadilishana uzoefu na wenye migodi mikubwa.


“Tuna vijana wameingia Tume ya Madini  bado hawajafahamu vitu vingi, hivyo ni fursa nzuri kwa  vijana katika sekta yetu kujifunza kupitia vikao kazi kama hivi,”amesema.


Amesema, sheria ya baruti ni ya muda mrefu hivyo wamejaribu kuona  ni namna gani wanaweza kuiboresha  ukizingatia wakati inatungwa na hali ya sasa ni tofauti kutokana na ongezeko la migodi.