Mbunge wa Jimbo la Lupembe, Wilaya ya Njombe,Edwin Swalle, amewatoa hofu wananchi wa jimbo hilo kuhusu mpango wa ujenzi wa barabara ya lami yenye urefu wa kilomita 42 kutoka Kibena hadi Kidegembye, akisisitiza kuwa utekelezaji wa mradi huo uko mbioni kuanza katika awamu ya kwanza.
Akizungumza leo mbele ya wananchi wa Kijiji cha Nyombo, kata ya Ikuna, Swalle amewahakikishia wananchi kuwa Serikali ina nia ya dhati ya kuboresha miundombinu ya usafirishaji katika maeneo ya vijijini ili kurahisisha shughuli za kiuchumi na kijamii.
“Serikali yenu sikivu imesikia kilio cha muda mrefu cha wananchi wa Lupembe kuhusu barabara hii. Niwahakikishie kuwa hatua za mwanzo za utekelezaji zimekamilika na muda wowote kazi itaanza. Tuendelee kuiamini Serikali yetu,” amesema Swalle.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Njombe, Mhandisi Charles Masuka, amethibitisha kuwa maandalizi yote muhimu yamekamilika kwa ajili ya kuanza kwa mradi huo wa kimkakati.
“Serikali kupitia TANROADS imekamilisha taratibu zote za kiutendaji na kisheria. Kile kilichosubiriwa kilikuwa ni hatua za mwisho tu za kiutekelezaji. Hivi karibuni kazi rasmi ya ujenzi itaanza,” amesema Mhandisi Masuka.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED