Wizara ya Afya imeikabidhi Halmashauri ya Manispaa ya Kahama lita 3,000 za dawa ya kuua mazalia ya mbu, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria.
Akizungumza na Nipashe Digital, Mratibu wa Udhibiti wa Wadudu katika Halmashauri hiyo, Nathanael Mganda, amesema dawa hizo zimetolewa kwa ajili ya kuongeza ufanisi katika zoezi la kunyunyizia dawa kwenye mazalia ya mbu sambamba na kuhimiza usafi wa mazingira na matumizi sahihi ya vyandarua vyenye dawa.
Mganda ameeleza kuwa katika mwaka wa fedha 2023/2024, halmashauri ilitenga bajeti ya Shilingi milioni 4.7 na kununua lita 360 za dawa kwa ajili ya kuua mazalia ya mbu. Hata hivyo, mwaka huu wa fedha 2024/2025, wamepata msaada wa lita 3,000 kutoka wizara, jambo alilosema litaongeza nguvu katika mapambano hayo.
“Dawa hizi tunazitumia kunyunyizia kwenye madimbwi na maeneo yenye mazalia ya mbu, lakini pia tunaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya vyandarua vilivyotolewa bure na serikali,” amesema Mganda.
Ameongeza kuwa mwezi Februari mwaka huu, halmashauri ilipokea vyandarua 328,479 kutoka serikalini na kuvigawa kwa kila kaya, sambamba na utoaji wa elimu kuhusu matumizi yake sahihi. Alisema elimu hiyo imesaidia kupunguza imani potofu kuwa vyandarua hupunguza nguvu za kiume au vinafaa kufugia kuku na samaki.
“Elimu tunayotoa imewasaidia wananchi kubadili mtazamo hasi kuhusu vyandarua. Sasa wanavitumia kwa matumizi sahihi na wakati huohuo tunapulizia dawa kwenye madimbwi kuua mbu kabla hawajazaliana,” amesema Mganda.
Aidha, ameeleza kuwa halmashauri hiyo imeanzisha utaratibu wa usafi wa mazingira kila siku ya Jumamosi ambapo kila kaya huhimizwa kusafisha maeneo yao kwa kina, kufukia madimbwi ya maji na kutumia vyandarua vyenye dawa.
Kwa upande wao, baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Kahama wamepongeza jitihada hizo na kueleza namna wanavyoshiriki kikamilifu katika shughuli za usafi na uelimishaji wa matumizi ya vyandarua.
Mkazi wa Kata ya Nyihogo, Abdully Athumani, alisema familia yake ilipatiwa elimu juu ya matumizi sahihi ya vyandarua, na sasa wameitikia kwa vitendo kwa kushiriki usafi kila Jumamosi na kufukia madimbwi yanayosababishwa na shughuli za ujenzi.
Naye Kasigwa Adamu, mkazi wa Majengo, alieleza kuwa yuko tayari kushirikiana na mamlaka za serikali kuwachukulia hatua wale watakaotumia vyandarua kwa matumizi yasiyokusudiwa.
“Endapo nitamuona mtu anawafungia kuku kwenye vyandarua vya bure vilivyotolewa na serikali, nitatoa taarifa kwa mamlaka husika ili hatua zichukuliwe. Kufanya hivyo ni kuivunja nguvu serikali katika jitihada zake za kulinda afya ya wananchi,” amesema Kasigwa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED