Wafanyabiashara Kariakoo wadai fidia ya bilioni 40 jengo kuporomoka

By Imani Nathaniel , Nipashe
Published at 01:45 PM May 29 2025
Wafanyabiashara Kariakoo wadai fidia ya bilioni 40 jengo kuporomoka

Wakili Peter Madeleka leo amezungumza na vyombo vya habari katika viunga vya Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam – Divisheni ya Ardhi, kuhusu kesi ya wafanyabiashara waliopata hasara kubwa kufuatia kuporomoka kwa jengo la ghorofa lililokuwa katika eneo la Kariakoo.

Kesi hiyo, ambayo leo ilikuwa imepangwa kwa ajili ya kupata amri mbalimbali muhimu kutoka kwa Mahakama, inahusu madai ya fidia ya shilingi bilioni 40 inayodaiwa na wafanyabiashara 50 wakiongozwa na Kanali Naftali Swali. Wadai hao walikuwa wakifanya biashara katika jengo hilo kabla ya kuporomoka mnamo Novemba 16, 2024 katika Mtaa wa Mchikichi na Kongo, Kariakoo.

Wafanyabiashara hao wanawadai fidia wamiliki wa jengo hilo ambao ni Leondela Mdete (49), mkazi wa Mbezi; Zenabu Islam (61) maarufu kama Zaibanu, mfanyabiashara mkazi wa Kariakoo; na Ashour Awadh Ashour (38), mfanyabiashara mkazi wa Ilala.

Hata hivyo, kusikilizwa kwa kesi hiyo kumeahirishwa baada ya Jaji anayesikiliza shauri hilo kupata changamoto ya kiafya. Mahakama imepanga upya tarehe ya kutajwa kwa kesi hiyo kuwa Juni 27, 2025 saa tatu asubuhi.

Kwa mujibu wa Wakili Madeleka, kesi hiyo ni ya msingi kwa ajili ya kutafuta haki za wafanyabiashara waliopoteza mali na mitaji yao, huku akikazia kuwa ni wakati wa kuwajibisha wamiliki wa majengo kwa uzembe unaosababisha madhara kwa watu wengine.