BALOZI wa Finland nchini, Theresa Zitting amesema nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kukuza na kuwasaidia wabunifu na wajasiliamari kwa kwa kuwajengea msingi wa ushirikiano.
Balozi huyo ameyasema hayo leo mei 28 mkoani Dar es Salaam katika halfla ya 'communicating innovation' iliyoandaliwa na watu kutoka Finland ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha wiki ya nchi za Nordic. Maadhimisho hayo yaliangazia kwa kina uendelevu wa mabadiliko ya kidijitali, na ubunifu. Wadau mbalimbali walihudhuria ikiwamo wanafunzi, wajasiriamali, washauri wa startups, maofisa wa serikali, na waendelezaji wa mazingira ya ubunifu.
Balozi Zitting amesema ubunifu hauwezi kustawi bila ushirikishwaji na kwamba lengo lao ni kuangazia namna mtu anavyoweza kuboresha wazo lake la kibunifu na kuwavutia wafadhiri. "Ubunifu ni nguvu ya dunia nzima kwa sasa. Unatoa fursa mpya za ukuaji wa uchumi jumuishi, huduma bora kwa umma, na suluhisho kwa changamoto ngumu. Kuanzia teknolojia ya fedha, afya, kilimo hadi uvumbuzi wa kijani zana za kidijitali zinachochea maendeleo endelevu na kuunda ajira kwa kizazi kipya" amesema Balozi Zitting
Amesema nchi ya Finland na nchi zingine za Nordic, zimejifunza kuwa mazingira ya ubunifu yanaweza kustawi mahali penye fursa za kubuni mawazo, kujenga biashara, na kutatua matatizo halisi. Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Startup Association (TSA), Zahoro Muhaji, amesema watu wa Nordic hasa Finland wamefanya kazi kubwa katika kusaidia wabunifu na wajasiliamari nchini.
Amesema katika hafla hiyo pia walisikiliza mawazo ya wabunifu mbalimbali kutoka nchini na mshindi alipewa zawadi na kwamba lengo kuu lilikuwa ni kuwajengea uwezo na uzoefu wa kuelezea biashara na mawazo na namna wanavyoweza kupata msaada kutoka kwa wafadhili kupitia mawazo yao.
Mmoja wa Walio wasilisha wazo la bunifu yake Rebeka Kitenge amesema maonyesho hayo yamemfanya ajue jinsi ya kuwaslisha wazo kwa wawekezaji ili kupata msaada kutoka kwa wafadhili. Amesema baada ya kupata maoni kutoka kwa jopo la majaji sasa anaenda kuboresha kile alichoshauliwa katika ubunifu wake wa kutengeneza sabuni za maji za kufulia ili aweze kuwa na bidhaa itakayoleta ushindani kimataifa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED