Vijana watakiwa kuchangamkia fursa ya kuonyesha vipaji
By
Shufaa Lyimo
,
Nipashe
Published at 07:12 PM May 28 2025
Picha: Mpigapicha Wetu
Simon Msuva.
Vijana nchini wametakiwa kutumia ipasavyo fursa ya kuonyesha vipaji vyao katika bonanza la Safari Cup, litakalofanyika Mei 31, 2025 kwenye Uwanja wa Nyamagana, mkoani Mwanza.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, mchezaji wa timu ya Taifa (Taifa Stars) na klabu ya Al Najma ya Saudi Arabia, Simon Msuva, amesema bonanza hilo ni jukwaa muhimu la kuibua wachezaji chipukizi wenye uwezo wa kuunda kikosi cha taifa katika siku zijazo.
“Ninashukuru Kampuni ya Safari kwa kunichagua kuwa Mkuu wa Skauti wa soka katika mashindano haya. Ninaamini tutapata vijana wengi wenye vipaji, hasa ikizingatiwa kuwa Mwanza ni miongoni mwa mikoa inayozalisha wachezaji bora,” amesema Msuva.
Ameongeza kuwa Tanzania ina hazina kubwa ya vijana wenye vipaji vya michezo, lakini wengi wao hukosa fursa za kujitokeza kutokana na ukosefu wa wawezeshaji na miundombinu bora ya kukuza vipaji.
Kwa upande wake, Meneja wa Bia ya Safari, Pamela Kikuli, amewataka wadau wa soka na vijana wa Mkoa wa Mwanza kujitokeza kwa wingi kushiriki katika bonanza hilo, akisisitiza kuwa nafasi ni chache.
“Tulifanya bonanza la kwanza mkoani Mbeya ambapo tulipata timu 24 na vijana wengi wenye vipaji. Wikiendi hii tunakuja Mwanza na tumejipanga vizuri zaidi baada ya kubaini mapungufu ya mwaka jana,” amesema Kikuli. 1
Ameongeza kuwa mwaka huu kumefanyika maboresho makubwa kwenye maandalizi ili kuhakikisha kila mshiriki anapata nafasi ya kuonyesha uwezo wake mbele ya makocha na wawakilishi wa vilabu mbalimbali.
Naye Msemaji wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Cliford Mario Ndimbo, amesema TFF itaendelea kushirikiana na Kampuni ya Safari Lager katika kuinua vipaji vya vijana, na kuzihimiza taasisi nyingine kuiga mfano huo.
“Ninaipongeza Safari Lager kwa kuamua kufanya jambo kubwa kama hili ambalo lina mchango mkubwa katika maendeleo ya soka la vijana nchini,” amesema Ndimbo.
Bonanza la Safari Cup limeelezwa kuwa sehemu ya mkakati mpana wa kuinua michezo nchini kwa kutoa jukwaa la vijana kupata nafasi ya kutambulika na kuchukuliwa na vilabu vya soka ndani na nje ya nchi.