Spika Dk.Tulia: Kauli zinazotolewa na wabunge siyo msimamo wa Bunge

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 08:41 PM May 28 2025
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Tulia Ackson
Picha:Mtandao
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Tulia Ackson

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Tulia Ackson, amesema kuwa kauli na mitazamo inayotolewa na wabunge katika michango yao bungeni haipaswi kuchukuliwa kama msimamo rasmi wa Bunge.

Dk. Tulia alitoa kauli hiyo leo bungeni mara baada ya kupitishwa kwa makadirio ya bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

“Waheshimiwa wabunge, Ibara ya 100 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inawapa uhuru wa mawazo na majadiliano ndani ya Bunge,” alisema Dk. Tulia.

Aidha, alifafanua kuwa kifungu cha 3 cha Sheria ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge (Sura ya 289) kinatoa ruhusa ya uhuru wa majadiliano kwa wabunge, sambamba na masharti ya Katiba na kanuni za kudumu za Bunge, hasa Kanuni ya 71, ambayo inaelekeza namna ya kutoa hoja au michango.

Spika alieleza kuwa wakati wa mijadala kuhusu bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi (Mei 26–27) na ile ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, baadhi ya wabunge walitoa michango iliyokiuka masharti ya kanuni hiyo.

“Michango ya baadhi ya waheshimiwa wabunge iliashiria kukiuka masharti ya Kanuni ya 71. Nitumie fursa hii kuwakumbusha kuwa mnapaswa kuzingatia matakwa ya Katiba, Sheria, na Kanuni za Bunge wakati wa majadiliano yenu,” alisisitiza Dk. Tulia.

Spika pia alitoa wito kwa wabunge kuhakikisha michango yao inazingatia maadili, ikiepuka kauli ambazo zinaenda kinyume na Katiba, sheria, au kanuni za Bunge walizojiwekea.