Wanafunzi zaidi ya 3,000 kutoka shule 24 za sekondari, zilizopo vijijini wamefikiwa na huduma za mtandao, baada ya wadau kuwapatia kompyuta zenye vitabu na mitihani iliyopita.
Aidha, Mkurugenzi wa Tume ya Tehama Tanzania (ICTC), Dk. Nkundwe Mwasaga, amesema ili Watanzania wanufaike na uchumi wa kidijitali, wadau wanahitaji kuunganisha nguvu na kuijengea jamii uwezo wa kubuini masuluhisho yanayoendana na mazingira yao.
Akizungumza Dar es Salaam leo Mei 27, 2025 kwenye Kongamano la Nne la Shule ya Mitandao Jamii Tanzania (Tanzania School of Community Network), Mratibu na Mwenyekiti wa shule hizo, Dk. Jabhera Matogoro, amesema wanafunzi walionufaika na idadi ya shule kwenye mabano ni kutoka Kasulu (7), Kondoa (5), Nyasa (8) na Tarime (4).
“Kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, tumefanikiwa kupeleka kompyuta zenye maktaba ya maswali (past papers), pamoja na vitabu kwenye hizi shule. Mwanafunzi anajifunza na kufanya maswali, pale anapokwama anamshirikisha mwalimu wake kwa ajili ya usaidizi,” amesema.
Amesema maktaba hizo zimeongeza uwezo wa wanafunzi kujifunza na kupenda masomo yakiwamo ya sayansi, ikilinganishwa na ilivyokuwa awali.
Dk. Matogoro ambaye pia ni mhadhiri wa katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), amesema utafiti alioufanya kwa miaka minane, umebaini kwamba Watanzania watanufaika zaidi na uchumi wa kidijitali, kama masafa ya televisheni ambayo hayajatumika, yatatumiwa kufikisha mawasiliano ya intaneti.
Akifungua kongamano hilo, Dk. Mwasaga amesema mawasiliano kwa wote sio chaguo ni haki ya msingi, ndio maana serikali imeweka mkakati wa kufikisha huduma hizo hadi maeneo ya pembezoni.
Amesema kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi, Watanzania wengi bado wanaishi vijijini, ambako wanahitaji kufikiwa na huduma za mawasiliano yakiwamo ya intaneti.
“Serikali inatoa nguvu kubwa kwa vituo kama hivi ambavyo vinaanzishwa na wananchi wenyewe, kwa sababu tunaamini katika masuluhisho ya kidijitali yanayoanzia chini kuja juu,” anasema.
Amesema ubunifu wa majukwaa ya kidijitali katika ngazi ya jamii, yataharakisha Tanzania kufikia lengo lake la kunufaika na uchumi wa eneo hilo, miaka michache ijayo.
“Vituo kama hivi, vinasaidia kufikisha maandalizi hayo mikoani na kuwaonesha wananchi fursa zinazokuja na uchumia wa kidijitali nchini, Kikanda na Kimataifa,” amesema.
Kongamoano hilo limewakutanisha wabunifu, watunga sera, watafiti, wanachama wa shule hizo, kwa lengo la kubuni pamoja mbinu mbalimbali za kuziba pengo la kidijitali nchini.
“Ili kuziba pengo la kidijitali Tanzania, ni lazima tushughulikie pengo la upatikanaji (coverage) na lile la matumizi (usage gap). Siyo tu kwa kujenga miundombinu ya kidigitali, bali pia kuhakikisha jamii zina ujuzi, maudhui na nyenzo za kutumia mtandao kwa maana halisi,” amesisitiza Dk. Matogoro.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED