Katibu wa NEC Oganizesheni na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Issa Usi maarufu Gavu amesisitiza Watanzania kuendelea kukiamini chama hicho kwa kuwa kinaendelea na mipango yake ya kuwaletea wananchi maendeleo kwa kuwapatia wagombea wenye uwezo.
Ameyasema hayo leo wakati wa kongamano la Umoja wa Vijana wa chama hicho UVCCM Wilaya ya Temeke ambalo limefanyika kwa lengo la kuelezea utekelezaji wa ilani ya CCM 2020/25.
"Kupitia mabadiliko ya katiba ya chama chetu, itaiwezesha kuisimamia ipasavyo serikali kutekeleza miradi ya kijamii na ile ya kimkakati lengo likiwa ni kuharakisha maendeleo," amesema.
UVCCM Temeke imesema imeridhishwa na utekelezaji wa ilani hiyo, na kwamba Sh. Bilioni 900 zilizotolewa chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan zilisaidia kutatua changamoto ya uhaba wa madarasa katika vyuo na vyuo vikuu nchini.
Naye, Zena Mgaya Mwenyekiti wa CCM Temeke amekemea tabia ya baadhi ya vyama vya upinzani kutweza utu na kufanya vitendo ambavyo vina ashiria uvunjifu wa amani.
Ofisa mipango kutoka Manispaa ya Temeke Dk. Siriel Mchembe ambaye ni mlezi wa UVCCM Dar es Salaam amesema miaka minne ya uongozi wa Rais Samia vyuo vikuu vimenufaika kwa mikopo, na kwamba Temeke ilipokea zaidi ya Sh. Bilioni 268 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED