Namelock Sokoine ataka haki mchujo wagombea CCM

By Allan Isack , Nipashe
Published at 12:19 PM Jun 15 2025
Namelock Sokoine
PICHA: MTANDAO
Namelock Sokoine

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu Taifa (CCM), Namelock Sokoine,amewataka viongozi ndani ya chama wanaohusika kupendekeza majina ya wagombea na kufanya mchujo watende haki na kuepuka kupendelea baadhi ya watu na kuwakanyaga wengine.

"Tutende haki kwa wagombea wote na tusiwaumize au kuwakanyaga wengine kwa kutumia nafasi zenu na vyeo vyenu kuwapendelea baadhi ya wagombea kwa kuwa baada ya uchaguzi kuna maisha,"alisema.Aidha Namelock, alisema kuelekea uchaguzi mkuu wagombea,viongozi wa chama na wanachama wanapaswa kutambua kuwa wanakwenda kugombea sio kugombana.

1


Alisema hayo jana  jijini Arusha,wakati wa akipokelewa kwenye ofisi za chama  Mkoa wa Arusha baada Mwenyekiti wa CCM Taifa Dk.Samia Suluhu Hassan kumteua kuwa Mjumbe  wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu Taifa.

“Tusiumizane katika chaguzi tupo viongozi hapa ambao tutashiriki katika nafasi za ndani katika michujo tusitumie nafasi zetu kukanyaga wenzetu ambao hawapo katika vikao hivyo, namshukuru Rais Samia kwa kuniteua katika nafasi hii,"alisema. 


Hata hivyo, ataitumikia nafasi hiyo, kwa uaminifu,uadilifu na unyenyekevu wa hali ya juu na kuwawakilisha vyema wanachama wa CCM na wananchi wa Mkoa wa Arusha.

Pia aliahidi kumsaidia kwa uaminifu Mwenyekiti wa CCM Taifa wakati akitekeleza majukumu yake, huku akitoa shukrani za dhati kwa kumchagua kushika nafasi hiyo.

Naye, Mwenyekiti CCM Mkoa wa Arusha, Thomas ole Sabaya, amempongeza Namelock kwa kuteuliwa katika nafasi hiyo, ya kuwa sehemu ya watoa uamuzi ngazi ya juu ya chama.

Alisema kihistoria ardhi ya Wilaya ya Moduli imetoa viongozi makini akiwemo Mawaziri Wakuu Hayati Edward Moringe Sokoine na Edward Lowassa na kwa sasa Namelock anafuata njia hiyo kwa kuwa ni mwanamke jasiri na mwenye msimamo.

Vilevile alisema kuteuliwa kwake kuwa  Mjumbe wa Kamati Kuu ni mwendelezo wa uaminifu na Mwenyekiti wa CCM Taifa kwa watu wa  Monduli na Mkoa wa Arusha kwa ujumla.