Jamii yashauriwa kujenga utamaduni kusafisha fukwe

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 03:53 PM Jun 15 2025
Jamii yashauriwa kujenga utamaduni kusafisha fukwe
PICHA: MTANDAO
Jamii yashauriwa kujenga utamaduni kusafisha fukwe

Jamii imeshauriwa kujenga utamaduni wa kufanya usafi katika fukwe ili kuvutia watalii na kujiepusha na maradhi.

Wito huo ulitolewa jana na Mratibu wa Data kutoka Taasisi ya Nipefagio inayojihusisha na Utunzaji wa Mazingira, Tajaeli Masaki wakati wakifanya usafi katika fukwe ya Kawe mkoani Dar es Salaam.
Amesema ni muhimu jamii kuendelea kutunza vyanzo vya maji na kulinda mazingira katika fukwe hiyo, kwa kuwa inatumiwa na watu wengi na shughuli mbalimbali za kiuchumi zinaendelea ikiwamo uvuvi.
“Tumechagua eneo hili ili kutunza mazingira na kuhakikisha lina baki salama, hali ilikuwa mbaya sana tumeokota taka nyingi za plastiki ambazo zinaharibu ikolojia ya bahari.
“Kufanya usafi kwenye fukwe ni pamoja na kuyatunza mazingira yake, katika eneo la kawe asilimia kubwa tumeokota taka za plastiki na chupa za rangi pamoja na vifungashio vya plastiki kama mifuko ya nailoni.
“Matumzi makubwa ya plastiki ndio sababu ya kuwapo kwa taka hizo katika fukwe na hivyo jamii inapaswa kutumia taka zinazoweza kurejelezwa iwe kuepuka uchafuzi wa mazingira” amesema Masaki
Mwenyekiti wa Mtaa wa Mzimuni Kawe, Raia Nasoro alifurahi kutembelewa na taasisi hiyo iliyoshirikiana na Muda Africa kufanya usafi katika fukwe hiyo kwa kuwa ni chanzo cha mapato kama ilivyo kwa vyanzo vingine vya kitalii.
Ameyaomba mashirika mengine kujitokeza kusaidia usafi katika fukwe hiyo huku akiwataka watanzania kujenga utamaduni wa kutunza fukwe ili kuendelea kuweka mazingira safi.
Juma Nasoro, Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), mabaye ni miongoni mwa walioshiriki kufanya usafi katika fukwe hiyo amesema ameguswa na suala hilo kwa kuwa ni la kimazingira.
Amesema hata wao, huwa wanashiriki kusafisha fukwe japo mwamko ni mdogo na kwamba huwenda wengi wao wana uelewa ndogo kuhusu umuhimu wa usafi wa mazingira.
Maiko Songoro, kutoka Muda Africa amesema wameamua kushirikiana na taasisi ya Nipefagio kwa kuwa lengo lao kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kufanya usafi katika fukwe.
Mwisho