Bodaboda, bajaji wazindua chama chao cha kukopa

By Renatha Msungu , Nipashe
Published at 02:51 PM Jun 13 2025
Bodaboda
PICHA: MTANDAO
Bodaboda

WANACHAMA wa Chama cha Waendesha Bodaboda na Bajaji Jiji la Dodoma (UMAPIDO) wametakiwa kukopa fedha kwenye chama chao kwa masharti nafuu na kujikwamua kiuchumi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Chama cha Akiba na Mikopo (SACCOS) cha umoja huo juzi, Mwenyekiti wa UMAPIDO, Chacha Marwa, alisema uamuzi wa kuanzisha kwake umetokana na mateso waliokuwa wakiyapata kutokana na mikopo kandamizi ya kausha damu.

 "Tunaishukuru sana COOP Bank (Benki ya Ushirika nchini)  na mlezi wetu wa SACCOS, Mheshimiwa Anthony Mavunde  kwa kutusaidia kuanzisha SACCOS hii. Tunaamini itatutoa kwenye mikopo umiza na ile ya 'kausha damu'," alisema Marwa.

 Akizungumzia kuhusu athari za mikopo hiyo ya awali ya kausha damu, Marwa alisema: "Tulikuwa tunakopeshwa Sh. 100,000, tunatakiwa kurejesha hadi Sh.300,000 na kushindwa kujiendeleza na wengine kukimbia kazi zao kwa kuogopa wadai."

 Aliendelea kusema kuwa wameamua kuachana na mikopo hiyo kandamizi kwa kuanza kujikopesha kupitia SACCOS hiyo kwa masharti nafuu ili kila mwanachama ajiinue kiuchumi. Akizindua SACCOS hiyo,  Mavunde,  Waziri wa Madini,  aliwataka wanachama hao kutumia fursa hiyo kujiunga na chama hicho.

 "Naomba nitoe wito kwa wote ambao bado si wanachama wa UMAPIDO, waichangamkie fursa hii kumiliki vyombo vyenu vya moto kupitia mikopo nafuu ya badala ya kukimbilia mikopo ya 'kausha damu' ambayo inawaumiza zaidi," alisema Mavunde ambaye ni  Mbunge wa Dodoma Mjini (CCM).

 Mkuu wa Idara ya Masoko na Mikopo wa COOP Bank, Yahya Kyoba, alisema wamejipanga kuwainua wafanyabiashara kwa kuwapatia mikopo nafuu itakayowawezesha kupiga hatua katika shughuli zao.