SIKU UCHANGIAJI DAMU DUNIANI, Muhimbili yahitaji chupa 150 kila saa 24

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 05:25 PM Jun 13 2025
Wajitokeza kuchangia damu
Picha: MNH
Wajitokeza kuchangia damu

Kila siku Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), inahitaji zaidi ya chupa 150 za damu, ili kukidhi mahitaji ya wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji, wanaojifungua, watoto wachanga na waathiriwa wa ajali.

Mhamasishaji wa Uchangiaji Damu kutoka MNH, Richard Msam, amesema hayo leo, Dar es Salaam, kuelekea Siku ya Uchangiaji Damu Duniani, kesho, iliyoandaliwa na hospitali hiyo, huku wafanyakazi wa kampuni ya Kefa wakichangia chupa 31.

Amesema malengo ya maadhimisho hayo ni kuokoa maisha ya maelfu ya wagonjwa wanaohitaji damu kwa dharura katika hospitali hiyo, kila siku.

“Mahitaji ya damu katika hospitali hiyo ni makubwa kutokana na idadi kubwa ya wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo kila siku. Kwa siku tunahitaji zaidi ya chupa 150 za damu, ili kukidhi mahitaji ya wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji, akinamama wanaojifungua, watoto wachanga na wahanga wa ajali mbalimbali,” amesema Msam.

Mkuu wa Idara ya Mawasiliano kampuni hiyo, Deogratius Chacha, amesema kampuni imetambua umuhimu wa damu salama katika kuokoa maisha na hivyo kuamua kushiriki kikamilifu katika kuchangia damu.

“Tunatambua kuwa damu haiwezi kutengenezwa viwandani, bali hutolewa na binadamu kwa hiari. Kwa sababu hiyo, tumepata fursa ya kutoa mchango wetu katika kuokoa maisha. Tunatoa wito kwa jamii nzima kujitokeza kuchangia damu mara kwa mara,” amesema.

Kauli mbiu ya mwaka huu ya maadhimisho ya Siku ya Uchangiaji Damu Duniani ambayo inaadhimishwa kesho, ni 'Changia Damu, Leta Matumaini pamoja, Okoa Maisha', ikiwa na lengo la kuhamasisha jamii kushiriki kwa hiari katika zoezi la uchangiaji damu.