Wizara ya Nishati, kwa ushirikiano na Modern Energy Cooking Services (MECS) na UK International Development, wamezindua rasmi Kampeni ya kwanza ya Kitaifa ya Uhamasishaji wa Nishati ya Umem ya Kupikia (eCooking) nchini Tanzania.
Mpango huo wa kihistoria ni sehemu ya Mpango wa MECS wa kukuza na kusaidia nishati ya umeme unaofadhiliwa na UKAid, ambao unatekelezwa nchini Tanzania ili kuharakisha mabadiliko ya matumizi ya kuni na mkaa kwenda kwenye matumizi ya umeme kwa shughuli za kupikia.
Kampeni hiyo inaunga mkono moja kwa moja Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi wa Kupikia wa 2024–2034, unaolenga kufikia asilimia 80 ya kaya kutumia mbinu safi za kupikia ifikapo 2034.
Lengo la awali la kampeni hiyo ni kufikisha uelewa kuhusu faida za nishati ya umeme kupikia kwa asilimia 80 ya wakazi wa maeneo ya mijini na pembezoni mwa miji kufikia Novemba 2025.
Akizungumza kabla ya uzinduzi huo jana jijini Dar es Salaam, Angellah Kairuki, Mshauri Maalum wa Rais wa Masuala ya Nishati Safi ya Kupikia na Maendeleo ya Jamii, alisema:
"Mabadiliko ya Tanzania kuelekea kupikia nishati safi si suala la nishati pekee, bali linagusa afya ya jamii, uhifadhi wa mazingira, uwezeshaji wa kiuchumi na usawa wa kijinsia. Kwa miongo mingi, jamii zetu zimekuwa zikibeba mzigo wa kutafuta kuni na mkaa kwa umbali mrefu, hali inayochangia magonjwa ya njia ya upumuaji, ukataji miti ovyo na umasikini." alisema na kuongeza kuwa;
"Kupitia kampeni hii ya kitaifa, tunapiga hatua jasiri kubadilisha namna Watanzania wanavyopika, tukitumia mtandao wetu wa umeme unaokua na Mkakati mpya wa Nishati Safi ya Kupikia ili kukuza suluhisho za kisasa, nafuu na endelevu. Hili ni suala la kutoa nafasi ya maisha bora na yenye heshima zaidi kwa kila kaya, hususan wanawake na watoto.” alisema
Dk. Anna Clements, Mtafiti Mkuu wa Mpango wa MECS nchini Tanzania, aliongeza:
"Tuna furaha kuunga mkono Tanzania katika kuchunguza njia mpya za kupikia zinazotoa urahisi zaidi na mbadala safi, huku zikiheshimu mila na desturi za watu. Kadri umeme unavyopatikana zaidi na vifaa vinavyokuwa rahisi kutumia, kaya nyingi zaidi zitagundua faida za njia za kisasa za kupikia zinazokidhi maisha ya kila siku. Kazi yetu ni kusaidia mazingira yatakayorahisisha uchaguzi huu na kuufanya uvutie zaidi.”
Kwa upande mwingine, Balozi Mkazi wa Uingereza nchini Tanzania, Marianne Young akizungumza kwa niaba ya UK International Development, ambaye ni mshirika mkuu, alisisitiza umuhimu wa kupikia nishati safi katika kufanikisha malengo ya maendeleo ya kimataifa, hasa katika usawa wa kijinsia na mabadiliko ya tabianchi.
"Kampeni hii ni hatua muhimu kwa malengo ya nishati na afya ya Tanzania. Inawahamasisha wananchi kufikiria namna mabadiliko madogo kwenye tabia za kupikia yanavyoweza kuleta manufaa makubwa, si kwa kubadili chakula chao, bali kwa kuwapatia chaguzi bora zaidi kwa familia zao na mazingira. Tunakaribisha kila mmoja — jamii, vyombo vya habari na wadau — kushiriki kusambaza uelewa na kuunga mkono mabadiliko haya chanya.”
Kampeni hiyo itatekelezwa kwa kutumia mfumo wa mikakati ya miji, ikianza na Dar es Salaam na baadaye kuenea kwenye miji mingine mikuu. Kupitia maonesho ya wazi, mikutano ya kijamii, mitandao ya mabalozi wa ndani na kampeni za vyombo vya habari, kampeni hii itaonesha namna kupikia kwa umeme kunavyoweza kuwa salama zaidi, nafuu na endelevu kwa kaya za Kitanzania.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED