Mafunzo kwa Wataalamu wa Mkoa na Halmashauri ya Manispaa ya Temeke kuhusu Utekelezaji wa Kampeni ya Huduma za Msaada wa Kisheria

By Imani Nathaniel , Nipashe
Published at 05:02 PM Jun 14 2025
Mafunzo kwa Wataalamu wa Mkoa na Halmashauri ya Manispaa ya Temeke kuhusu Utekelezaji wa Kampeni ya Huduma za Msaada wa Kisheria
PICHA: IMANI NATHANIEL
Mafunzo kwa Wataalamu wa Mkoa na Halmashauri ya Manispaa ya Temeke kuhusu Utekelezaji wa Kampeni ya Huduma za Msaada wa Kisheria

Katibu Tawala Msaidizi wa Miundombinu Mkoa wa Dar es Salaam, Amani Mafuru, amewataka washiriki wa mafunzo pamoja na wataalamu wa ngazi ya Mkoa na Halmashauri ya Manispaa ya Temeke kutumia weledi wao katika kutatua changamoto zinazowakabili wakazi wa jiji la Dar es Salaam, hasa katika mchakato wa utekelezaji wa Kampeni ya Huduma za Msaada wa Kisheria ya Mama Samia.

Ameyasema haya wakati akifungua mafunzo yanayofanyika jijini Dar es Salaam yanayowalenga wataalamu mbalimbali, kwa lengo la kuwajengea uwezo katika utoaji wa huduma za kisheria zitakazotolewa kwenye viwanja vya wazi vya Mbagala kupitia mabanda ya maturubai.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Msaada wa Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Ester Msambazi, amesema kuwa kampeni hiyo itatekelezwa katika pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  yaani Tanzania Bara na Zanzibar.

 Msambazi alieleza kuwa kikao hiki ni muhimu kwa kuwa kinatoa fursa ya kubadilishana ujuzi na mikakati ya pamoja katika utekelezaji wa kampeni, sambamba na kuwajengea wataalamu uwezo wa kukabiliana na changamoto mbalimbali ndani ya jamii. "Wataalamu tunaokutana nao leo ni kwa ajili ya kuwajengea uwezo juu ya namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali ndani ya jamii zetu," alisisitiza.