MSANII wa muziki wa Bongo Fleva, Lady Jaydee, amesema siri ya mafanikio yake katika sanaa ya muziki ni kuwa imara na kuamini katika kile anachokifanya.
Ameeleza hayo juzi jijini Dar es Salaam katika Ukumbi wa Super Dome Masako wakati tamasha lake la kutumiza miaka 25 ya uimbaji. Alisema watanzania wanapaswa kuheshimi sanaa na kuiona kama kazi zingine, kwamba ameielekeza miaka 25 ya uimbaji wake kwa mama yake mzazi, aliyemlea na Rais Samia Suluhu Hassan.
Jaydee alisema kuwa kila msanii anapokuwa anaanza huwa na matumaini makubwa kuhusu mafanikio ya baadaye, ambapo juhudi, nguvu na kujituma ndizo zilizomsaidia kufanikisha ndoto zake na kufika alipo sasa. Aidha, amewahimiza wasanii wa kike nchini, hasa mabinti, kujiamini kwani hilo ni jambo la msingi kwa yeyote anayetaka kudumu kwa muda mrefu katika tasnia ya muziki.
Naye, Mtendaji wa Baraza la Sanaa Tanzania ( Basata), Dk. Kedmon Mapana akizungumza wakati wa tamasha hilo alisema sanaa siyo uhuni wala kupoteza muda kama watu wanavyodhani bali ni kazi inayomuingizia mtu kipato na heshima katika jamii.
Dk. Mapana alisema kwa miaka yote Jaydee hajawahi kutoka kwenye game amekuwa ni mwanamuziki aliye juu kimuziki na sisi Basata tunampongeza kwa juhudi hizo. "Sanaa ni maisha kama maisha mengine. Sanaa ni sawa na mtu aliyesoma kuwa daktari au mwanasheria. Leo Lady Jaydee ameuthibitishia umma kuwa sanaa ni kazi kama kazi zingine," alisema Dk. Mapana.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED